Kontena Lenye Meno ya Tembo Lakamatwa Zanzibar

Kontena Lenye Meno ya Tembo Lakamatwa Zanzibar

Kontena Lenye Meno ya Tembo Lakamatwa Zanzibar

JUHUDI za kupambana na wasafirishaji nyara za Serikali na wahujumu uchumi nchini Tanzania zimezidi kuzaa matunda, baada ya shehena nyingine ya meno ya Tembo kukamatwa na Jeshi la Polisi Mjini Zanzibar.

Akizungumzia tukio hilo, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema meno hayo yamekamatwa yakiwa kwenye kontena lenye urefu wa futi 40, huku wasafirishaji wakijifanya kutaka kusafirisha makombe ya konokono wa baharini.

Kamishna Mussa alisema meno hayo ya tembo yalikuwa yamefungwa kwenye mifuko huku yakiwa yamechanganywa na makombe ya konokono ndani ya kontena tayari kwa kusafirishwa kwenda nje ya nchini.

Hii ni mara yapili Serikali kukamata shehena kubwa ya meno hayo kwa kipindi kifupi, kwani hivi karibuni mjini Dar es Salaam, polisi tena walikamata shehena kubwa ya meno ya tembo (meno 706 ya tembo, sawa na tembo 353 waliouawa) yakiwa yamefichwa katika moja ya nyumba walimokuwa wanakaa raia wa Kichina.

Watu wawili wamekamatwa wakihusishwa na meno hayo.

Kukamatwa kwa meno haya ya tembo, kumekuja wakati tayari serikali imetangaza kusitisha Operesheni Tokomeza Ujangili, ambayo ililenga kunusuru wanyama walio hatarini kutoweka kutokana na kuuawa katika hifadhi za taifa nchini Tanzania. Wanyama wanaolengwa zaidi na majangili kutokana na meno yao na pembe ni tembo na faru.

Matukio ya kukamatwa kwa meno ya tembo kutoka Afrika Mashariki yamekuwa yakiripotiwa kila mara. Oktoba, 20, 2012, tani nne za meno ya tembo yenye thamani ya dola milioni 3.4 za Kimarekani yalikamatwa Hong Kong, yakidaiwa kusafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.

Pia Agosti 16 mwaka huu polisi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata raia wa Vietnam akiwa na meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 18 sawa na dola zaidi ya elfu 11, yakisafirishwa kwenda nje.