RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameirudishia Kampuni ya Nyamigogo Grand Vezir Holdings ya Mkoani Geita zawadi ya gramu 227 za dhahabu safi akielekeza kuwa zawadi hiyo itumike kuwasaidia watoto yatima.
Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo, Novemba 11, 2013, baada ya kukabidhiwa zawadi ya dhahabu hiyo wakati wa sherehe ya kuzindua mgodi wa uchenjuaji dhahabu wa kampuni hiyo nje kidogo ya mji mdogo wa Kharuma ambako ndiko makao makuu ya wilaya mpya ya Nyang’hwale, Mkoa wa Geita. Gramu hizo 227 ambazo ni sawa na aunzi nane zina thamani ya Sh. milioni 16 kwa bei ya sasa ya soko la dhahabu duniani.
Baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo, Rais Kikwete ameuliza: “Sasa nifanye nini na zawadi hii? Nawarudishieni hii dhahabu, iuzeni popote mnakotaka na fedha itakayopatikana tutawapa watoto yatima.”
Akizungumza na wananchi katika mgodi huo, Rais Kikwete ameupongeza uongozi wa mgodi huo akisema kuwa umeongeza thamani ya dhahabu na ya maisha ya wananchi katika eneo hilo nje ya mji mdogo wa Kharuma.
Hata hivyo, Rais Kikwete ameushauri uongozi wa mgodi huo kufanya jitihada za kuboresha teknolojia inayotumika. “Mmefanya vizuri sana na mgodi huu ni mradi wa maana sana kwa kuongeza thamani ya dhahabu na kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hili. Ubunifu huu unastahili pongezi.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Lakini lazima tuboreshe teknolojia. Teknolojia inayotumika kwenye mgodi huu bado ni ya zamani kidogo. Hii ni sawa na hadithi ya mtu mwenye chongo katika jamii ya vipofu watupu. Yeye anaonekana kama mfalme.”
Mgodi wa Nyamigogo ambao ni mgodi wa marudio kwa maana ya kwamba unazalisha dhahabu kutokana na mchanga ambao huko nyuma umepata kufuliwa na kutoa dhahabu, ulianzishwa mwaka 2011 na mpaka sasa zimewekezwa kiasi cha Sh. bilioni 1.6 katika uendelezaji wa mgodi huo. Risala ya uongozi wa mgodi huo inasema kuwa mgodi huo unaozalisha kiasi cha gramu kati ya 500 na 600 kwa mwezi na unaajiri watu 45 wakiwemo wanawake 10.
Tokea kuanzishwa kwake, mgodi huo umekuwa unaunga mkono shughuli za jamii inayouzunguka ikiwa ni pamoja na kujenga zahanati na madarasa ya shule katika vijiji viwili. Rais Kikwete amezindua mgodi huo ikiwa sehemu ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika ziara yake rasmi ya kikazi katika Mkoa wa Geita, moja ya mikoa minne ambayo aliianzisha mwaka jana. Mikoa mingine ni Simiyu, Njombe na Katavi.
Ziara hiyo ya siku tano inamalizika kesho, Jumanne, Novemba 12, 2013, na mbali ya kuzindua mgodi huo, Rais Kikwete leo amepokea ripoti ya maendeleo ya Wilaya ya Nyang’hwale na kuhutubia mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Kharuma uliohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi.