RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake inaelekeza nguvu nyingi na kasi mpya katika umeme kwa sababu hakuna nchi iliyopata kuendelea kwa kutumia koroboi ama karabai.
Aidha, Rais Kikwete ametaka vyombo vinavyohusika na kusambaza na kuunganisha umeme katika vijiji mbali mbali nchini kuongeza kasi ya kufanya kazi kwa sababu ni lazima vijiji 1,600 vipate umeme katika muda mfupi.
Rais Kikwete ameyasema hayo Jumapili, Novemba 10, 2013 wakati alipozungumza na wananchi katika eneo la Buseresere/Katoro, mpakani mwa wilaya za Geita na Chato, Mkoa wa Geita ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika Mkoa wa Geita ambako amekuwepo kwa siku tatu. Buseresere na Katoro ni miji iliyoungana lakini Buseresere iko Wilaya ya Chato na Katoro iko Wilaya ya Geita.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza na mamia kwa mamia ya wananchi kabla ya kuzindua mradi mkubwa wa kusambaza umeme katika vijiji vya wilaya nne za Mkoa wa Geita na moja ya Mkoa wa Shinyanga. Umeme unasambazwa katika vijiji 14 vikiwamo 10 vya Wilaya ya Geita.
Umeme huo ni sehemu ya miradi mikubwa ya miundombinu ya umeme, barabara, maji na Uwanja wa Ndege wa Mafia inayogharimiwa na Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) la Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Milenia Tanzania (MCA-T).
Mradi huo wa kusambaza umeme katika vijiji vya wilaya za Geita, Chato na Nyang’hwale Mkoani Geita na Msalala (Shinyanga) umegharimu dola za Marekani 21, 477, 181 (sawa na Sh. Bilioni 36.3) na utanufaisha wateja 3,500 katika maeneo hayo.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake imeamua kuelekeza nguvu nyingi katika kusambaza umeme vijijini kwa sababu umeme ndiyo maendeleo.
“Hakuna nchi iliyopata kuendelea duniani kwa kutumia koroboi ama karabai. Nchi zote zilizoendelea zimefanya hivyo kwa kutumia umeme na kuwekeza ipasavyo katika sekta hiyo ya umeme.”
Akijibu malalamiko ya wananchi kuwa usambaza wa umeme huo unachelewa pamoja na kwamba wamelipia kuunganishiwa umeme, Rais Kikwete ameziekeleza taasisi zinazohusika na kazi ya kusambaza na kuunganisha umeme.
“Mmesikia wenyewe malalamiko ya wananchi kwamba kasi ya kuunganisha umeme siyo kubwa. Napenda tuongeze kasi kwa sababu tunayo kazi kubwa ya kusambaza umeme katika vijiji 1,600 vya nchi yetu katika muda mfupi ujao. Hivyo, tunongeze kasi ili tuweze kuikamilisha kazi hiyo mapema iwezekanavyo.”
Rais Kikwete pia amewaambia wananchi kuwa ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya umeme kwa urahisi, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imepunguza ada za kuunganisha umeme kutoka sh. 450,000 hadi 170,000.
Mapema leo, Rais Kikwete amezindua mradi wa maji wa Masumbwe katika kijiji cha Shinyanga A, wilaya mpya ambazo ziliundwa na Rais Kikwete mwaka jana.Mradi huo uliogharimu Sh. Milioni 341 ni moja ya miradi ya maji katika vijiji 10 kila mkoa inayogharimiwa na Benki ya Dunia (WB).
Rais Kikwete pia amezindua Wodi ya Wazazi katika kituo cha afya cha Kijiji cha Iboya, Kata ya Mbogwe. Mradi huo umegharimu Sh. Milioni 57 na ujenzi wa wodi hiyo ni maandalizi ya kukifanya kituo hicho cha afya hospitali mpya ya wilaya mpya ya Mbogwe.
Wakati huo huo; RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Novemba 9, 2013, ameweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara nyingine muhimu ikiwa ni barabara ya pili kuwekewa jiwe la msingi katika siku mbili za mwanzo za ziara ya Rais Kikwete mkoani Geita.
Baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Bwanga-Biharamulo jana, Ijumaa, Novemba 8, 2013, kwenye siku ya kwanza ya ziara yake, leo Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi la ujenzi kwa kiwango cha lami la Barabara ya Iyovu-Bwanga.
Barabara ya Bwanga-Biharamulo ambayo sherehe za uwekaji jiwe lake ulifanyika kwenye Kijiji cha Buziku, Tarafa ya Bwanga, ina kilomita 67 na ni barabara nyingine ambayo inaunganisha mikoa ya Kagera na Geita.
Barabara hiyo inayojengwa na kampuni ya Sinohydro ya China inagharimu Sh. Bilioni 54.76 na inatarajiwa kuwa imekamilika Februari mwaka 2015.
Sherehe za uwekaji jiwe la msingi kwenye Bararaba ya Iyovu-Bwanga zimefanyika kwenye Kijiji cha Iyovu, Kata ya Runzewe na kuhudhuriwa na mamia kwa mami ya wananchi.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 45 inajengwa kwa kiasi cha Sh. Bilioni 43.36 na inatarajiwa kumalizika Agosti, mwakani, 2014.