Tanzania Haitajitoa Uanachama EAC Ng’o – Rais Kikwete

Rais Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema nchi ya Tanzania haitajitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) licha ya vitendo vya ‘ubaguzi’ vinavyofanywa na baadhi ya nchi wanachama wa umoja huo kwa kuitenga Tanzania. Kauli hiyo imetolewa leo na Rais Kikwete alipolihutubia Bunge la Tanzania mjini Dodoma jioni hii. Akizungumza katika hotuba yake amesema kutohusishwa kwa Tanzania katika baadhi ya mikutano iliyofanywa na baadhi ya wanachama wa EAC yaani nchi za Kenya, Uganda na Rwanda hakuikatishi tamaa.

“…Nimeona nifanye hivyo kutokana na maswali mengi ambayo Watanzania wanajiuliza kufuatia matukio ya hivi karibuni ya viongozi wa nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Uganda, Rwanda na Kenya kukutana bila ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania na Burundi. Viongozi wenzangu hao wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe 24-25 Juni, 2013 mjini Entebbe, Uganda; tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa, Kenya; na tarehe 28 Oktoba, 2013 mjini Kigali, Rwanda.” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alionesha kushangazwa na vikao vilivyofanyika na kuitenga Tanzania kana kwamba ndio kikwazo katika jumuiya. Alisema Kwa mujibu wa matamko ya pamoja (Communique) yaliyotolewa baada ya mikutano hiyo, iliyofanywa na nchi hizo wameamua mwambo nane pasipo kuihusisha Tanzania na mengine yamo katika ushirikiano wa EAC.

Alisema mambo waliokubaliana bila uwepo wa Tanzania katika mkutano wao ni pamoja na kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura, ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini, kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda na kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote.

Rais Kikwete aliongeza mengine ni kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho, Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist Visa), Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao na mwisho ni kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.

“Ni dhahiri kwamba orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na yale yasiyo ya Jumuiya. Kwa mfano, mambo manne kati ya hayo manane hayamo kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au kupata ridhaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jambo la kwanza ni uzalishaji na usambazaji wa umeme. Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa na akiba ya pamoja ya nguvu ya umeme (East African Power Pool). Hata hivyo, bado jukumu la kuzalisha na kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama zenyewe kuamua. Lakini, hivi ndugu zetu hawa wanao muhali kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sote ni wanachama?”

“Lazima nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila sababu ya kuuliza kwa nini wenzetu wameamua kufanya hivi. Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha Aprili 28, 2013 na Juni 24, 2013 walipokutana kuamua kufanya mambo ya kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kubaguana, Haijawahi kuwa hivi kabla.” Alisema Rais Kikwete katika hotuba hiyo.

“…Mheshimiwa Spika; Katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa utaratibu wake wa utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hatuna maneno nayo. Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria na Visa ya Pamoja ya Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa tayari waanze. Lakini, kwa upande wa kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory) na Shirikisho la Afrika Mashariki tunadhani wenzetu wamekiuka uamuzi wetu wa pamoja.

Aidha alisema Tanzania haijafanya jambo lo lote baya dhidi ya Jumuiya au nchi yoyote mwanachama, na ni mwanachama mvumilivu, mtiifu na mwaminifu kwa Jumuiya hivyo kushangazwa na hatua inayoendelea kwa wanachama wengine. Alibainisha kuwa Tanzania inatimiza ipasavyo wajibu wake kwa Jumuiya na kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wake na utengamano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“…Mheshimiwa Spika; Kwa kweli huwa najiuliza maswali mengi na kukosa majibu kuhusu nini kinachoendelea kufanywa na viongozi wenzangu watatu na kwa nini! Nakosa majibu ya uhakika. Je wenzetu wamekosa imani na Jumuiya ya Afrika Mashariki na je wanataka kuunda yao? Je wanaichukia nchi yetu na hivyo wameamua kutufanyia vitimbi tutoke! Au sijui wanachuki na mimi! Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa hatuna mpango wa kutoka (kama vijana wasemavyo hatoki mtu hapa). Tupo na tutaendelea kuwepo!” alisema JK.