TANZANIA ni miongoni mwa nchi tano za Afrika ambazo zimejitolea kutoa askari wa kuunda Kikosi cha Kukabiliana na Migogoro ya Kijeshi Barani Afrika cha African Capacity for Immediate Response to Crises (ACIRC) kitakachoundwa kwa mujibu wa uamuzi wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).
Tanzania itatoa kikosi kimoja (Battalion Group) na nchi nyingine ambazo zimekubali kuchangia askari ama polisi katika Kikosi hicho ni Afrika Kusini, Uganda, Algeria na Chad. Nchi hizo zilijitokeza kushiriki katika Kikosi hicho wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Majeshi wa nchi hizo uliofanyika Jumapili iliyopita mjini Pretoria, Afrika Kusini, mkutano ambao maamuzi yake yameidhinishwa na kukubaliwa na wakuu wa nchi akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete. Wakuu hao walikutana Pretoria, Novemba 5, 2013.
Uamuzi wa kuanzisha Kikosi hicho ulitolewa na Wakuu wa Nchi wanachama wa AU waliokutana katika kikao chao cha 22 cha kawaida mwezi Mei, mwaka huu, 2013, mjini Addis Ababa. ACIRC kitakuwa kikosi cha muda wakati Afrika inaendelea na maandalizi yake ya kuunda Jeshi la Kudumu la Afrika (Africa Standby Force) na Lenye Uwezo wa Kukabiliana na Migogoro Haraka na Popote (Rapid Deployment Force).
Jeshi hili litakuwa ni jeshi lenye uwezo wa kuingia nchi yoyote, chini ya AU, na hivyo wakati mwingine litatumika kutuliza migogoro katika nchi yoyote ya Afrika hata kama nchi husika haijaomba msaada wa jeshi hilo. Jeshi hilo litakalofanya kazi yake chini ya mfumo wa Amani na Usalama katika Afrika – African Peace and Security Architecture (APSA) litaiwezesha AU kuwa na jeshi la askari na polisi wenye uwezo na nguvu kukabiliana na mizozo ya kijeshi barani humo na kuwa vifaa vyake vitatolewa nchi wanachama wa AU ambao watakuwa tayari kushiriki katika mpango huo.