Baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Pongwe pawani wakichukua jeneza lenye mwili wa Marehemu Baba yake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, wakati wa maziko yaliyofanyika Kijijini hapo, Wilaya ya Kati Unguja.[Picha na Ramadhan Othman, Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Shein akimfariji Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai baada ya kufiliwa na baba yake mzazi, na kuzikwa katika kijiji cha Pongwepwani Wilaya ya Kati Unguja.[Picha na Ramadhan Othman, Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Shein (wa tatu kulia) akijumuika na Waislamu mbalimbali na Viongozi kubeba jeneza la Marehemu Baba yake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, baada ya kumswalia katika Msikiti wa Ijumaa na kuzikwa Pongwepwani.[Picha na Ramadhan Othman, Ikulu.]
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai, kufuatia kifo cha baba yake mzazi, Mzee Ali Vuai, kilichotokea usiku wa Novemba 5, 2013, mjini Zanzibar.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa majonzi na mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha baba yako, Mzee Ali Vuai, ambacho nimejulishwa kuwa kimetokea usiku wa kuamkia leo mjini Zanzibar ambako pia naambiwa maziko yamefanyika leo hii.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kwa niaba ya uongozi wa Chama chetu, wanachama wake, makada na mashabiki wake wote na kwa niaba yangu mimi mwenyewe, nakutumia wewe Mheshimiwa Vuai Ali Vuai, Naibu Katibu Mkuu wetu, salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo cha mzee wetu huyu. Napenda kukujulisha kuwa sisi sote ndani ya CCM tuko nawe katika kipindi hiki cha majonzi makubwa ya kuondokewa na mzazi wako. Tunaelewa machungu na majonzi yako na tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu akupe nguvu na uvumilivu kuweza kuvuka kipindi hiki.”
Rais Kikwete amemalizia salamu zake: “Aidha, kwa pamoja tuko nawe katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema roho ya Marehemu Mzee Ali Vuai.”