Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (wa tatu mstari wa mbele kulia) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya ujumbe kutoka Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu na baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (katikati) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) akifafanua jambo kuhusu wanawake wa Tanzania wanavyokabiliwa na ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti wakati wa mazungumzo baina yake na baadhi ujumbe kutoka Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Na Anna Nkinda- Maelezo
TAASISI ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) kwa kushirikiana na Utepe wa Pink Utepe Mwekundu (PRRR) wanatarajia kuanza kufanya kazi kwa pamoja ya kuhakikisha ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi na matiti unapungua au kuisha kabisa hapa nchini.
Hayo yamebainishwa leo wakati wa mazungumzo baina ya Wafanyakazi wa Taasisi ya WAMA wakiongozwa na Mwenyekiti wao Mke wa Rais Mama Salma Kikwete na Ujumbe kutoka Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu yaliyofanyika katika ofisi za WAMA zilizopo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji kutoka Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu Dk. Doyin Oluwole alisema jambo la muhimu ni kuangalia jinsi gani wanaweza kufanya kazi kwa pamoja na kuweza kuudhibiti ugonjwa huo ambao unawatesa wanawake wengi hapa nchini.
“Ili kukabiliana na ugonjwa huu Serikali ya Marekani kupitia Mpango wa dharula wa kupunguza makali ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi (PEPFAR) imetoa dola za kimarekani millioni tatu kwa kipindi cha miaka mitano na mashine 16 za cryotherapy kwa ajili ya kusambaza huduma za upimaji na tiba kwa wanawake wenye ugonjwa saratani ya shingo ya kizazi”, alisema Dk, Doyin.
Pia kwa kipindi cha miaka mitatu Shirika la Misaada la Marekani (UNAIDS) limetoa dola 33,000 kwa ajili ya kusaidia ushiriki wa wanawake wenye VVU na kufanya kazi na vikundi vidogovidogo katika jamii. Taasisi ya Bristol –Myers Squibb kwa kipindi cha miaka mitatu imetoa dola za kimarekani milioni 1.2 kwa ajili ya kusaidia huduma za kuhamasisha jamii kuhusu vikoba na kuimarisha huduma za jamii.
Alisema watashirikiana kwa kila hali ili kuhakikisha kuwa wanawake wa Tanzania wanapata matibabu ya ugonjwa huo lakini hawawezi kufanya kazi peke yao bila ya Mama Kikwete kwani yeye ni mama wa taifa, akiongea na wanawake watamsikiliza.
Aidha Dk. Oluwole pia alimpongea mama Kikwete pamoja na mmewe Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwasaidia watanzania.
Dk. Doyin alisema, “Tunakupongeza kwa kazi kubwa unayoifanya ya kutumia sauti yako kuwaelimisha watanzania kuhusiana na mambo mbalimbali ya maendeleo, kuhusu ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti sisi tukiongea na watanzania hawatatuelewa kama vile wewe ukisimama na kuongea nao”.
Kwa upande wake Mama Kikwete aliishukuru Serikali ya Marekani kwa misaada mingi wanayoitoa kwa wananchi wa Tanzania na kusema kama ushirikiano huo utaanza kufanya kazi mapema itakuwa ni rahisi kuweka kukabiliana na ugonjwa huo ambao unaua wanawake wengi hapa nchini.
Mama Kikwete alisema hivi sasa maambuki ya Ugonjwa wa Ukimwi yamepungua kwa asilimia 5.1 lakini kuna mikoa ambayo bado maambukizi yako juu kama mkoa wa Njombe kwa asilimia 14.8, Iringa, Mbeya na Mwanza.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema changamoto iliyopo ni kuwa mtu mwenye viashiria vya kupata ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ana hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU hali hiyo haiwezi kufumbiwa macho ni lazima ipatiwe ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano jambo ambalo litapunguza tatizo hilo kwa kiasi kikubwa.
“Tunatambua kwamba saratani ya shingo ya kizazi inaua wanawake wengi hapa nchini, mwanamke anakitu kinaitwa usiri anaweza kupata tatizo akakaa nalo kwa muda mrefu na kuona aibu kulisema ingawa inaweza kutokea kwa bahati mbaya mtu mwingine akaona kuwa kuna tatizo lakini bado mwanamke huyo akashindwa kusema.
Ni muhimu tukawaelimisha wanawake wakajua kuna ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti, tatizo si kujua tatizo lililopo bali tatizo ni kuficha ugonjwa naamini wakati umefika wa kulifanyia kazi jambo hili ni muhimu kuangalia mahali ambako kuna tatizo kubwa zaidi na kupeleka utetezi kwa wahusika kwani maisha bora ya watanzania yanategemea kuimarika kwa afya zao nchi ikiwa na watu wenye afya njema kutakuwa na kizazi chema pamoja na viongozi wazuri hapo baadaye”, alisema Mama Kikwete.
Utepe wa Pink Utepe Mweupe ni muungano wa mashirika ya kiserikali na yale yasiyo ya Kiserikali ya nchini Marekani wenye malengo yanayofanana ya kupunguza vifo vitokanavyo na saratani ya shingo ya uzazi na ile ya matiti katika nchi zenye uchumi wa chini na ule wa kati. Washirika wa muungano huo ni Chuo cha George W. Bush, PEPFAR, UNAIDS, Susan G Komen, Becton Dickinson na Kampuni yake, Taasisi za a Bill ma Melinda Gates, Bristol Meyers Squibb na Caris, IBM, Merck , Qiagen, Taasisi ya Taifa ya Saratani, Medisend, AirBarneLife Line, MD Anderson, Jamii ya Kansa ya Marekani na American Society for Clinical Pathology.
Tanzania ni nchi ya tatu katika nchi za Afrika kuingia kwenye urafiki na Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu ambao ulizinduliwa na Rais Dk. Kikwete na Rais Mstaafu wa Marekani George W. Bush kwenye mkutano wa wake wa Marais wa Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam katikati ya mwaka huu. Utafanya kazi chini ya uongozi wa mkakati wa taifa wa upimaji na uzuiaji wa saratani ya shingo ya uzazi na dira ya wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.