JK Aomboleza Kifo cha Jaji Mstaafu Hillary Mkate

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa heshima za mwisho kwa Marehemu Jaji Mstaafu Hilary Mkate leo Oktioba 4, 2013 Kinondoni Dar es salaam

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa heshima za mwisho kwa Marehemu Jaji Mstaafu Hilary Mkate leo Oktioba 4, 2013 Kinondoni Dar es salaam

jk3
Rais Jakkaya Kikwete akimfariji Mwenyekitio wa Tume ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva baada ya kuaga mwili wa marehemu Jaji Mstaafu Hilary Mkate leo Oktoba 4, 2013 Kinondoni, Dar es salaam. PICHA NA IKULU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu, Damian Z. Lubuva kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Wakili wa Kujitegemea, Jaji Mstaafu, Hillary Mkate kilichotokea nyumbani kwake Kinondoni Jijini Dar es Salaam tarehe 1 Novemba, 2013.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Hillary Mkate ambaye amewahi kuitumikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa uadilifu mkubwa, na hivyo kutoa mchango stahiki katika kuiongoza Tume hiyo kufanya kazi zake kikamilifu”, amesema kwa masikitiko Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.

Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Jaji Hillary Mkate, enzi za uhai wake, kama kiongozi mwadilifu na mchapakazi hodari ambaye alitumia vipaji vyake vyote alivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kutoa haki kwa wananchi mbalimbali waliokuwa wakizitafuta haki zao kutokana na sababu mbalimbali.

“Kutokana na msiba huu mkubwa, Ninakutumia wewe Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Damian Lubuva, Watumishi wote wa Mahakama na Wanasheria kote nchini kwa kuondokewa na mwenzao, Jaji Mstaafu na Wakili wa Kujitegemea, Mheshimiwa Hillary Mkate. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu, Amina”, ameongeza kusema Rais Kikwete.
Aidha Rais Kikwete amemuomba Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Damian Lubuva kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya Marehemu Jaji Mstaafu, Hillary Mkate kwa kupotelewa na Kiongozi na Mhimili wa Familia.

Amewahakikishia Wanafamilia hao kuwa yuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao. Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira katika kuomboleza msiba huu kwa vile yote ni Mapenzi yake Mola.