Waziri wa Kilimo, Eng. Christopher Chiza, akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais kufungua kongamano hilo.
Makamu wa Rais Dk. Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau waliohudhuria Kongamano hilo, baada ya ufunguzi. Picha na OMR.
Baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo, wakimsikiliza Makamu wa Rais wakati akisoma hotuba yake ya ufunguzi.
MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal ametoa changamoto kwa wawekezaji wa nje na ndani kuona fursa za uwekezaji katika sekta ya korosho kwani ni muda muafaka wa kuelekeza uwekezaji katika sekta hiyo ili kuzalisha na kuchakatua korosho zote kwa 100% ndani ya nchi.
Dk. Mohammed Bilal aliyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akifungua rasmi Kongamano la Sekta ya Korosho wa kujadili fursa za uwekezaji wa zao la korosho hapa nchini linalowashirikisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi, mkutano huo unafanyika kwa siku mbili Novemba 4 na 5, 2013 katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
“Tumekusanyika mahali hapa kujadili fursa mbalimbali zinazoweza kishirikisha Sekta binafsi kushiriki katika kukuza Sekta ya zao la korosho nchini hususani katika kuhakikisha inachukua nafasi yake katika maandalizi ya zao la korosho, upatikanaji wa masoko na huduma za kifedha ili kuleta mageuzi makubwa katika sekta muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu” alisema Dk. Mohammed Bilal.
Kongamano hilo lenye kauli mbiu ya “Wekeza katika ubanguaji wa korosho, Kuongeza Ajira na kuza uchumi” umeandaliwa na Jukwaa lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na Kilimo nchini (ANSAF), Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) na Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) linafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 4 mpaka 5 Novemba, 2013.
Watu zaidi ya 150 kutoka ndani na nje ya nchi wamepata nafasi ya kuhudhuria kongamano hilo kutoka sekta tofauti, washiriki hao wanajadili na kupanga mpango mkakati wa kutambua fursa mbalimbali zilizo katika zao la korosho, wadau hao pia watajadili jinsi ya kuongeza uwezo wa wakulima wadogo wa zao hilo hapa nchini. Dhima ya kongamano hilo kuangalia uwezekano wa kubangua zao la korosho ndani ya Tanzania ili kuongeza uzalishaji wa ndani na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.
Makamo wa rais alisema kwamba Katika mazingira ya sasa ambayo korosho inasafarishwa kama ilivyo, bado imebaki kuwa miongoni mwa mazao matatu ya juu yanayoliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni. Naamini mikakati ikiwekwa, likaandaliwa vyema na kusafirishwa, zao hili litaongoza kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni, sambamba na kutoa ajira za kutosha kwa vijana wetu na wanawake na kutengeneza soko la uhakika kwa wakulima wadogo.
Akizungumzia dhamira ya serikali katika kuboresha sekta ya korosho Mh. Makamu wa Rais alisema kuwa “Pamoja na matatizo yanayojiri, yamekuwepo mafanikio mazuri kwa sekta hii hususani katika uzalishaji wake na uandaaji na masoko. Haya ni matokeo ya dhamira ya kweli ya serikali na hatua mbalimbali inzochukua zikiwemo; kuboresha masoko na mfumo wa stakabadhi ghalani, kuimarisha bodi mablimbali na mamlaka zinaoshughulikia zao hili, ikiwemo Bodi ya Korosho Tanzania (CBT)”.
Naamini tutafanikiwa zaidi kama tutawahakikishia wazalishaji wa korosho kwamba mabadiliko endelevu yanayoendelea sasa yatakuwa na mafaniko makubwa kwa wakulima na suala zima la uchumi wa nchi yetu. Alisema makamu wa rais.
Mkutano wa uwekezaji wa zao la korosho umehudhuriwa na wadau kutoka sekta mbalimbali, wawekezaji wa ndani na nje, wakulima wadogo, vyombo vya kusimamia korosho, wabunge na mawaziri. Wote hawa wamekusanyika pamoja kupanga mikakati ya kuwezesha kuliweka zao la korosho katika sehemu inayostahili kuwepo katika uchumi wa Tanzania.
Mijadala ya mkutano huo imejikita zaidi katika kuzitambua na kuzijadili fursa zenye tija zilizopo kwenye zao la korosho ambalo linalimwa na baadhi ya jamii masikini nchini Tanzania. Kwa takwimu zilizopo hivi sasa zinaonyesha kuwa Tanzania inapoteza dola za Kimarekani 110 kwa mwaka kutokana na kusafirisha malighafi za zao la korosho na kupoteza ajira zaidi ya 45,000 ambazo zingesaidia wanawake na vijana kupata ajira. Ni dhahiri juhudi za washiriki wa mkutano huo ni kuona Tanzania inabangua korosho kwa asilimia 100 ndani ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa ANSAF, Ndg. Audax Rukonge alisema kwamba mkutano huo ni zao lillilotakana na utafiti ulifanyika na ANSAF kwa kushirkiana kwa karibu na Baraza la Kilimo Tanzania kuweza kuangalia usimamizi mzima wa zao la korosho utafiti uliodhaminiwa na BEST-AC. Utafiti huo ulilenga kutafuta njia sahihi za kuzitumia katika sekta ya korosho ili kuweza kuweka sekta hiyo sehemu sahihi.
Mkurugenzi huyo alisema kwamba “kwa muda mrefu sasa korosho ya Tanzania imekuwa katika maendeleo ya kusuasua japokuwa kuna sababu nyingi ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya kuzalisha na kubangua korosho ndani ya nchi. Sekta ya korosho imekuwa na mafanikio katika uzalishaji wa zao hilo huku wakulima wadogo ndio wakionyesha kuzalisha kwa kiasi kikubwa lakini sekta hiyo haijafika hatua ya maendeleo ambayo yanaweza kutarajiwa kutokana na thamani katika soko na uzalishaji pia”.
Ushauri mwingi umetolewa lakini suluhisho la mwisho ni kwamba Tanzania ni lazima ichakatue korosho ndani na kuuza bidhaa hiyo nje ya nchi kuliko kusafirisha malighafi ya zao la korosho. Hili ni swala la haraka kuweza kulishughulikia ili kuweza kutoa matokeo mazuri ya kuinua uchumi wa Tanzania na kuongeza ajira kwani kama zao hili litasimamiwa kwa umakini na kunavyostahili basi ajira nyingi zitaongezeka na kipato cha mkulima mdogo kuongezeka.
Mkutano wa uwekezaji katika sekta ya korosho umedhaminiwa na wadau wakubwa wa kilimo na zao la korosho ambao ni Benki ya NMB, LIMAS, Hansa-Diamond Motors, PASS, Mfuko wa Asasi za Kiraia,, OLAM na BEST-AC.