Serikali Yasema Haijafuta Daraja Ziro Kidato cha Nne..!

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo.

Na Joachim Mushi

SERIKALI imesema haijafuta daraja ziro kwenye mtihani wa taifa kama inavyo endelea kutafsiriwa na wananchi wengi mara baada ya kutoa viwango vipya vya madaraja ya ufaulu. Taarifa hiyo imetolewa hivi punde bungeni na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alipokuwa akitoa ufafanuzi wa swali na nyiongeza bungeni lililoulizwa kutaka ufafanuzi juu ya mabadiliko hayo ya viwango vya ufaulu.

Mulugo alisema Serikali haijafuta daraja sifuri kwenye mitihani hasa ya kidato cha nne bali kilichofanyika katika viwango vipya vya madaraja ya ufaulu yaliotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ni kuongeza madaraja ili kuboresha na kuwatendea haki watahiniwa kwenye mitihani hiyo.

“Mheshimiwa Spika swali lingine mheshimiwa anasema kushusha madaraja ya viwango vya ufaulu ndio suluhisho la kuwaokoa vijana wanaokuwa wamefeli mitihani yao..! Jibu hilo la hasha hatujashusha madaraja wala kubadili viwango vya ufaulu tofauti na ilivyokuwa bali tulichokifanya ni kuongeza madaraja ili kuwatambua watoto, kwamba awali kulikuwa na mlundikano wa alama katika daraja moja,” alisema Mulugo akifafanua zaidi.

Alisema ilichokifanya Serikali ni kuongeza madaraja ili kutawanya mlundikano wa alama katika daraja moja kitendo ambacho kilikuwa kikiwanyima haki baadhi ya watainiwa kwenye matokeo ya mitihani yao. “Mheshimiwa Spika kwa mfano Baraza la Mitihani lilikuwa linatumia F inaanzia sifuri mpaka 34 lakini unakuja kujiulinza tena kwa kuzingatia kuwa kulikuwa hakuna rekondi ya alama za ufaulu (continues assessment) tofauti na sera inavyoelekeza kwamba iwepo tena ya alama 50 kwa 50, yaani mtihani wa mwisho alama 50 na rekodi za ufaulu alama 50.

Alisema walichokifanya sasa mtihani wa mwisho utakuwa na alama 60 huku rekodi ya maendeleo ya mwanafunzi shuleni ikichukua alama 40 ili kupata alama zake sahihi katika mtihani wa mwisho. Aliongeza kuwa “…Sasa lipo suala la kujiuliza hivi hawa wanafunzi ambao walikuwa wanapata alama 34 je nao kweli wamepata ‘F’? Sasa tumezipanga tena zile alama na kuweka madaraja yatofautiane kwa alama kumi kumi, lakini hapa bado alama za ufaulu zitaendelea kuwa zile zile yaani alama 40 ndio kiwango cha ufaulu. Sio kweli kama watu wanavyosema kuwa kwa viwango vipya mwanafunzi akipata alama 16 na 20 eti amefaulu na anaenda kidato cha tano.

Alisema katika kufanya uchaguzi wa wanafunzi waliochanguliwa kuendelea na masomo utabaki vile vile kama awali lakini kwenye upangaji madaraja ndipo Wizara imeanzia daraja F, E, D, C, B, B+ na A ili kuondoa ulundikano wa alama kwenye daraja moja kama ilivyokuwa hapo awali. Alisema daraja sifuri litaendelea kuwepo na wala serikali haijalifuta kama ilivyo andikwa na vyombo vya habari.

Alisema kilichotokea ni mkanganyiko wa taarifa na tafsiri isiyo sahihi tofauti na malengo ya wizara hiyo. Aidha Spika aliishauri vizara hiyo kujipanga na kutoa taarifa ya Serikali ili kuondoa mkanganyiko uliopo katika suala hilo.