Simba na Kagera Waingiza Mil 32, TPL Board Yalaani Vurugu…!

TPL Board yalaani vurugu Michezoni

MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Kagera iliyochezwa jana (Oktoba 31 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 32,726,000. Washabiki waliohudhuria mechi hiyo namba 81 iliyomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 walikuwa 5,541 ambapo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 4,992,101.69, gharama za kuchapa tiketi sh. 3,183,890 wakati kila klabu ilipata sh. 7,242,252.45.

Wamiliki wa uwanja walipata sh. 3,682,501.25, gharama za mchezo sh. 2,209,500.75, Bodi ya Ligi sh. 2,209,500.75, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,104,750.37, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 859,250.29.

VPL YAENDELEA RAUNDI YA 12
Raundi ya 12 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ambayo ipo katika raundi yake ya 12 inaendelea kesho (Novemba 2 mwaka huu) kwa mechi nne zitakazochezwa katika miji minne tofauti.

Mgambo Shooting na Coastal Union zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Mbeya City na Ashanti United zitaumana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).

Raundi hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Tanzania Prisons itakuwa mwenyeji wa Oljoro kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7 mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashanti United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.

Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City, Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Rhino itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons.

Boniface Wambura Mgoyo, Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)