Sumbu Galawa Afariki Dunia, Ikulu Yamkumbuka

Rais Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Parseko Vicent Kone kuomboleza kifo cha kiongozi wa miaka mingi nchini, Sumbu Galawa ambaye ameaga dunia usiku wa Oktoba 30, 2013 akiwa na umri wa miaka 79.

“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za kifo cha Mheshimiwa Sumbu Galawa ambaye nimejulishwa kuwa ameaga dunia usiku wa saa saba kuamkia leo katika Hospitali ya Puma, Wilaya ya Ikungi, mkoani kwako Singida. Nakutumia wewe salamu zangu za rambirambi kuomboleza kifo cha Mtanzania mwenzetu ambaye alitumia vipaji vyake vyote katika utumishi wa nchi yetu na umma wake,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake na kuongeza:

“Mheshimiwa Sumbu Gawala alithibitisha uongozi wake na mapenzi yake kwa watu aliowatumikia katika nafasi zake zote ambazo alipata kuwa nazo katika maisha yake, iwe ni kwenye nafasi yake ya Ubunge wa Singida Mjini, ama kwenye Ukuu wa wilaya katika wilaya nyingi nchini, ama kwenye nafasi yake ya Uenyekiti wa Chama chetu katika Mkoa wako wa Singida ama kwenye Ukatibu wa Wilaya wa Chama. Ameaga dunia akiwa mfano wa kuigwa wa uongozi na ametuacha wakati bado tunahitaji sana busara zake muhimu.”
Amesema Rais Kikwete: “Kufutia msiba huo, nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Parseko Vicent Kone salamu zangu wa rambirambi na kupitia kwako kwa wananchi wote wa Singida, Chama chetu cha CCM kwa kuondokewa na kiongozi na mwanachama mwenzao.”

“Aidha, kupitia kwako nawatumia wanafamilia ya marehemu salamu za dhati ya moyo wangu na pole nyingi kwa kuondokewa na kiongozi na muhimili wa familia. Napenda wajue kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa na nawaombea nguvu ya Mwenyezi Mungu wawe na subira na uvumilivu katika kipindi hiki cha machungu na majonzi kwa sababu yote ni mapenzi ya Mungu. Wajulishe kuwa naungana nao katika kumwomba mwenyezi Mungu aiweke pema roho ya Marehemu Sumbu Galawa.
Amina.”