ASKOFU wa Jimbo la Kanisa Katoliki la Morogoro, Askofu Telesphory Mkude amemsifia na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuanzisha, kusimamia na kuongoza vizuri mchakato wa kutungwa kwa Katiba mpya nchini.
Pia Askofu Mkude amewataka wananchi badala ya kukaa na kulalamika, lazima wajitokeze na kutoa maoni yao ili kuboresha mchakato huo na kuiwezesha Tanzania kupata Katiba nzuri ambayo itaiongoza kwa miaka mingine 50 ijayo.
Aidha, Askofu mkude amemwelezea Rais Kikwete kama kiongozi wa mfano ambaye anawajali wananchi wake na kushirikiana nao katika kujitafutia maendeleo. Vile vile, Askofu Mkude amemsifia Rais Kikwete kwa kuendelea kusimamia na kudumisha amani nchini pamoja na changamoto kubwa na nyingi anazokabiliana nazo katika kutimiza wajibu wake huo kama kiongozi.
Askofu Mkude ametoa pongezi na sifa hizo jana, Jumapili, Oktoba 27, 2013 wakati alipotoa neno ya shukurani mwishoni mwa sherehe za miaka 100 za Parokia ya Lugoba, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani. Askofu Mkude amewaambia mamia kwa mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo kwenye Kanisa la Msalaba Mtukuka ambako pia kuna shule aliyosoma Rais Kikwete mwanzoni mwa miaka ya 1960:
“Umefanya mengi sana wakati wa kipindi cha uongozi lakini moja ya mambo hayo makubwa ni kuanzisha, kusimamia na kuongoza mageuzi makubwa ya kutungwa kwa Katiba mpya katika nchi yetu. Tunakupa heko sana kwa kusimamia jambo hili ambalo litatuwezesha sote kupata Katiba inayotokana na ridhaa ya wananchi.”
Miongoni mwa viongozi wa dini na kilei waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Askofu Anthony Banzi, Askofu wa Jimbo la Tanga.
Kuhusu nafasi ya wananchi katika mchakato huo, Askofu Mkude amesema: “Tuache kunung’unika. Tutoe mani ya kuboresha Katiba yetu. Si viongozi wengi wanatoa nafasi kama hii duniani kwa wananchi wao kushiriki katika kujadili Katiba yao wenyewe. Kama asingependa, Rais angeweza kubakia na Katiba ya sasa ambayo ni nzuri.”
Kuhusu suala la amani nchini, Askofu Mkude amesema kuwa ni muhimu kwa Watanzania kumuunga mkono Rais Kikwete katika kuibakiza Tanzania kisima cha amani katika eneo lililojaa mizozo na migogoro isiyoisha.
Amesisitiza: “Lakini wako wenzetu hapa nchini ambao pengine hawaelewi maana ya amani. Amani ni muhimu sana kwa mambo mengine yote. Tuacha malumbano na mapambano. Sasa sisi tukivurugana hapa tutakimbilia wapi? Tumezungukwa na vita kila upande, huko mashariki tuna bahari, sasa tutakwenda wapi tukiivuruga nchi yetu?”
Ameongeza Askofu, “Mheshimiwa Rais, napenda pia kukupongeza kwa kuwa karibu na wananchi na kushirikiana nao katika mikakati ya maendeleo. Hata kabla hujawa Rais, ukiwa bado Mbunge uliwafanyia mambo mengi na makubwa watu wako. Angalia ule mradi wa maji wa Chalinze, nani alikuwa anapata maji katika ukanda wetu huu?”
Mbali na kusoma katika Shule ya Kati ya Lugoba kati ya mwaka 1962 na 1965 wakati huo ikiitwa St. John Bosco’s Lugoba Middle School iliyokuwa inamilikiwa na Kanisa Katoliki, Rais Kikwete amekuwa anachangia maendeleo ya shule na Parokia ya Lugoba.
Hata kabla ya kuanza kwa sherehe za miaka 100 jana, Rais Kikwete alizindua rasmi zahanati ya Kanisa ambayo yeye mwenye alisaidia kuikarabati na pia aliweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Ukumbi ambao unajengwa na Parokia hiyo kwa gharama ya Sh. milioni 200.
Parokia ya Lugoba ilianzishwa miaka 100 na mapadre Cornel na Herman kwa kushirikiana na wenyeji akiwemo Mtawala wa eneo hilo wakati huo, Mzee Kinogile.