Na Anna Nkinda – Maelezo
RAIS wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete leo atakuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za mahafali ya kwanza ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo kijiji cha Nyamisati wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na kusainiwa na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ambayo ndiyo mmiliki wa shule hiyo, Daudi Nasib inasema jumla ya wanafunzi wa kike 67 wanatarajia kuhitimu elimu yao ya kidato cha nne Novemba mwaka huu.
Taarifa inasema shule ya Sekondari ya WAMA – Nakayama ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Taasisi ya WAMA na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi wenye mapenzi ya kusaidia jamii. Bodi ya Wakurugenzi ya WAMA iliamua Shule hiyo iitwe jina hilo kwa heshima ya Bwana Hayao Nakayama kutoka Japani aliyetoa msaada uliosaidia ujenzi wa awamu ya kwanza ya shule.
“Moja ya malengo ya Taasisi ya WAMA ni kusaidia upatikanaji wa Elimu bora ya Sekondari kwa watoto wa kike na watoto wengine waishio katika mazingira hatarishi na yatima. Na ni kwa mantiki hii ndiyo maana shule ya WAMA – Nakayama imejengwa ili kutimiza lengo hili.
Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA, Mama Salma Kikwete na Bodi ya Wakurugenzi ya WAMA inapenda kutoa shukrani za dhati kwa wadau wote wanaosaidia Shule ya WAMA – Nakayama na kuunga mkono juhudi za Taasisi yetu”, ilisema taarifa ya Nasib.
Shule ya Sekondari ya WAMA – Nakayama ilianza mwaka 2010 ina wanafunzi wa kike 325 kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ambao ni yatima na wengine wanatoka familia maskini, watoto hawa wasingeweza kupata elimu ya sekondari bila ya msaada wa Taasisi ya WAMA ambayo huwapatia mahitaji yao yote bure ikiwemo; malazi, chakula, sare za shule, shajara, vitabu na nauli za kwenda makwao kipindi cha likizo.
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ni Taasisi isiyo ya kiserikali na isiyo ya kibiashara iliyoanzishwa na Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, mwaka 2006 ina malengo ya kuboresha maisha ya wanawake na wasichana katika masuala ya afya, elimu na uchumi pamoja na kutengeneza fursa za maendeleo ya wakina mama na watoto.