Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanahabari wakimsikiliza Tenga katika mkutano wake na wanahabari hao.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Ofisa habari wa TFF, Bonifasi Wambura na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah (kulia)
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema ataendelea kufanya kazi ya kuinua mpira wa miguu nchini licha ya kumaliza muda wake kesho kutwa. Tenga ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Makao Makuu ya TFF, jijini Dar es Salaam kutolea ufafanuzi masuala kadhaa ikiwemo maangalizi ya Mkutano Mkuu wa taasisi hiyo na mwenendo wa uchaguzi utakaofanyika kwenye mkutano huo.
Alisema kumaliza muda wake haiwezi kuwa mwisho wa yeye kufanya kazi za mpira wa miguu nchini, kwani ataendelea na mchakato wa kuinua soka kuanzia ngazi za chini kuandaa vijana na kutafuta udhamini utakaoliinua soka la Tanzania.
“Sita subiri kupewa kazi kama mlivyouliza…nitaendelea kufanya kazi ya kuinua soka letu maeneo mbalimbali,” alisema Tenga alipokuwa akijibu swali la mmoja wa waandishi kama atakuwa tayari kufanya kazi kwenye kamati yoyote ndani ya TFF endapo ataombwa kufanya hivyo.
Aidha Tenga alikiri kufurahishwa na jinsi kampeni za uchaguzi zinazokwenda kutoka na ukweli kuwa wagombea wamekuwa wakielezea kile wanachotaka kuufanyia mpira wa miguu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF leo mchana, Rais Tenga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) amesema Watanzania wanataka kusikia ajenda za wagombea.
“Ombi langu ni kwamba kampeni zimeanza vizuri, watu wanazungumza hoja zaidi. Ni jukumu la wajumbe kupima na kufanya uamuzi. Kwangu mimi nimejitayarisha kumkabidhi Katiba, Rais mpya wa TFF,” amesema.
Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) amesema kazi kubwa iliyofanywa na uongozi wake ni kujenga taasisi (TFF) pamoja na kuweka mifumo (structure) inayoainisha majukumu ya kila mmoja.
“Ajenda yetu wakati tunaingia madarakani mwaka 2005 ilikuwa ni kujenga taasisi. Tayari taasisi ipo, sasa mtazamo uwe kuushughulia mpira wa miguu wenyewe,” amesema.
Mkutano Mkuu wa TFF unafanyika kesho kwenye ukumbi wa mikutano wa NSSF Waterfront, na tayari wajumbe wa mkutano huo ambao pia utakuwa na ajenda ya uchaguzi siku inayofuata wameshawasili jijini Dar es Salaam.
Wawakilishi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ashford Mamelodi ambaye ni Ofisa Maendeleo wa kanda hii, Magdi Shams El Din ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) ni miongoni mwa wageni watakaohudhuria mkutano huo.