IKIWA ni siku kadhaa baada ya kuibuka tuhuma za wanajeshi kupora vitu kadhaa katika uvamizi wa maduka ya Westgate, Wakuu wa idara ya Polisi nchini Kenya wamewaonya waandisi wa habari kuhusu walivyoripoti matukio katika sakata hilo lililosababisha mauaji, kujeruhi na uharibifu mkubwa.
Onyo hili linakuja baada ya taarifa za wanajeshi kufanya uporaji katika jengo hilo wakati wakipambana na magaidi hao waliokuwa wamewateka nyara watu waliokuweme ndani ya jumba hilo kubwa la maduka.
Mkuu wa polisi, David Kimaiyo alisema kuwa waandishi hawapaswi kutoa habari au kuchochea propaganda, au kuwachochea Wakenya wakati wakipeperusha matangazo yao.
Duru zinasema kuwa baadhi ya waandishi wa habari wamehojiwa na polisi leo kuhusiana na sakata hilo.
Picha za CCTV zilizofichuliwa kwa waandishi wa habari zilionesha wanajeshi wakitoka ndani ya jumba hilo na mifuko ya plastiki iliyoshukiwa kuwa na bidhaa kutoka katika mojawapo ya maduka makubwa yaliyokuwa ndani ya jengo hilo la Nakumatt.
Hata hivyo jeshi limekanusha madai hayo na kusema kuwa wanajeshi walikuwa wanachukua maji ya kunywa wakati wa operesheni yao dhidi ya magaidi.
Takriban watu 67 walifariki ikiwemo wanajeshi na mamia ya wengine kujeruhiwa kwenye shambulizi hilo lililofanywa na wanamgambo wa Al Shabaab kama walivyokiri. Waliwateka nyara watu ndani ya jengo hilo kwa siku nne.
Pamoja na kupora, vyomo vya habari Kenya vimesema kuwa baadhi ya wanajeshi waliuwana na wenzao wakati wa operesheni yao kutokana na kile kilichosemekana kuwa ukosefu wa maelekezo mazuri kutoka kwa wakuu wa usalama.
-BBC