Taarifa mbalimbali muhimu kutoka TFF leo


Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura’

STARS KUCHEZA PALESTINA, JORDAN

Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Tanzania (Taifa Stars) itakuwa na ziara ya
mechi mbili nje ya nchi. Stars itacheza mechi ya kwanza Agosti 10 mwaka huu
mjini Ramallah, Palestina dhidi ya timu ya Taifa ya nchi hiyo.

Stars ambayo inatarajia kuondoka Agosti 7 mwaka huu kwa ajili ya ziara ya mechi
hizo mbili, itacheza mechi ya pili Agosti 13 mwaka huu dhidi ya Jordan katika
Jiji la Aman.

Kocha Mkuu wa Stars, Jan Poulsen ambaye hivi sasa yuko likizo kwao Denmark
anatarajia kutangaza kikosi chake kwa ajili ya maandalizi ya mechi hizo mara
baada ya kurejea nchini mapema mwezi ujao.

SEMINA, MITIHANI KWA WAAMUZI

Semina na mitihani ya utimamu wa mwili (physical fitness test) kwa waamuzi wa
daraja la pili na tatu itafanyika katika vituo vya Dodoma, Mwanza na Ruvuma
kuanzia Agosti 2-5 mwaka huu.

Waamuzi husika watajitegemea kwa usafiri, chakula na malazi. Tunavikumbusha
vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kuwajulisha wahusika ili washiriki semina na
mitihani ambayo pia itatumika kuwapandisha madaraja wale watakaofaulu.

Semina kama hiyo kwa waamuzi wa daraja la IA na IB iliyoanza Julai 13 mwaka huu
inaendelea katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza na itamalizika kesho (Julai
16 mwaka huu).

TWIGA STARS- MAPUTO 2011
Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) itaanza
mashindano ya All Africa Games yatakayofanyika Septemba mwaka huu jijini Maputo,
Msumbiji, Septemba 5 kwa kupambana na Ghana.

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo iliyotolewa jana Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF), Twiga Stars ambayo iko kundi B itacheza mechi ya pili
Septemba 8 mwaka huu kwa kupambana na Afrika Kusini kabla ya kumaliza hatua ya
makundi Septemba 11 mwaka huu dhidi ya Zimbabwe.

Mechi za nusu fainali zitachezwa Septemba 13 na 14 mwaka huu wakati ile ya
kutafuta mshindi wa tatu itakuwa Septemba 16 mwaka huu na fainali ni Septemba 17
mwaka huu. Timu mbili za kwanza katika kila kundi ndizo zitakazofuzu kwa hatua
ya nusu fainali.

Kundi A katika michuano hiyo lina timu za wenyeji Msumbiji, Cameroon, Algeria na
Guinea. Nigeria ndiyo waliokuwa mabingwa wa 2007, lakini hawakufanikiwa kufuzu
kwa michuano hiyo mwaka huu ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne.

Boniface Wambura