RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema kufuatia kifo cha aliyepata kuwa Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Mstaafu, James Kombe aliyefariki dunia tarehe 22 Oktoba, 2013 katika Hospitali ya Ocean Road iliyoko Jijini Dar es Salaam akipatiwa matibabu.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha aliyepata kuwa Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani hapa nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Mstaafu, James Kombe aliyefikwa na umauti akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Ocean Road Jijini Dar es Salaam” amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
“Nilimfahamu Marehemu James Kombe, enzi za uhai wake, kama Askari Shupavu, Mtiifu na Mwaminifu aliyejituma vilivyo katika utekelezaji wa majukumu yake. Kwa hakika sifa hizi ndizo zilizochangia kwa kiasi kikubwa kupandishwa Cheo na kushika nyadhifa mbalimbali za juu hadi kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD); Mkuu wa Polisi wa Mkoa (RPC); Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), na hatimaye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, cheo alichokitumikia hadi alipostaafu mwaka 2010”, ameongeza kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Rais Kikwete amesema utumishi huu uliotukuka wa Kamanda James Kombe ndani ya Jeshi la Polisi, ni wa kujivunia na wa kupigiwa mfano ambao Askari Polisi wengine hawana budi kuuiga ili Jeshi letu la Polisi liendelee kuaminiwa, kuheshimiwa na kupewa ushirikiano stahiki kutoka kwa Wananchi.
“Kutokana na Msiba huu, ninakutumia Salamu za Rambirambi wewe Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema kwa kumpoteza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Mstaafu, Marehemu James Kombe. Natambua fika kuwa licha ya kustaafu kwake, ushauri wake kwa Jeshi letu la Polisi ulikuwa bado unahitajika sana”, ameongeza kusema Rais Kikwete.
Aidha Rais Kikwete amemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema kumfikishia Salamu zake za Rambirambi kwa Familia ya Marehemu James Kombe. Ameihakikishia Familia hiyo kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza kifo cha Kiongozi na Mhimili Madhubuti wa Familia yao.
Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu James Kombe. Ameiomba Familia ya Marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na ujasiri wakati huu inapopitia machungu ya kuomboleza Msiba wa Mpendwa wao.