Rais atoa Rambirambi za Msiba wa “Uncle J. Nyaisanga”

20131021-163123.jpg

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara kufuatia kifo cha Mtangazaji Mkongwe hapa nchini na aliyekuwa Mkurugenzi wa Abood Media inayomiliki Kituo cha Televisheni cha Abood, Bwana Julius Nyaisanga maarufu kwa jina la Uncle J. Nyaisanga.

Bwana Nyaisanga aliyewahi kufanya kazi Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo hivi sasa ni TBC Taifa, na katika Kampuni ya IPP Media ambako alikuwa Mkurugenzi wa Radio One, alifariki dunia tarehe 20 Oktoba, 2013 katika Hospitali ya Mazimbu iliyoko katika Manispaa ya Morogoro alikopelekwa kupatiwa matibabu ya ugonjwa wa kisukari.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa kutokana na kifo cha Mtangazaji Maarufu na Mkongwe hapa nchini katika Tasnia ya Habari hususan upande wa Utangazaji, Bwana Julius Nyaisanga kwani kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa katika Tasnia hiyo”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.

Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Julius Nyaisanga enzi za uhai wake kama Mtangazaji aliyekuwa na bidii kubwa ya kazi na mwenye sauti iliyokuwa na mvuto mkubwa kwa wasikilizaji katika sehemu zote alizowahi kufanyia kazi.

“Kwa hakika mchango wa Marehemu Julius Nyaisanga kwa maendeleo ya Taifa letu kupitia Utangazaji, ni mkubwa na wa kupigiwa mfano ambao sote kama Taifa hatuna budi kujivunia”, ameongeza kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.

“Kutokana na msiba huu mkubwa, ninakutumia wewe Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara Salamu zangu za Rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa Watangazaji Maarufu na Wakongwe hapa nchini. Aidha kupitia kwako naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya Marehemu Julius Nyaisanga kwa kuondokewa na Mhimili na Kiongozi wa Familia”.

Rais Kikwete amewahakikishia Wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa. Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu na subira wakati huu wanapopita katika kipindi kigumu cha kuomboleza kifo cha mpendwa wao. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu Julius Nyaisanga.

Vilevile Rais Kikwete ametoa pole kwa Waandishi wa Habari na Watangazaji kote nchini kwa kumpoteza Mwanataaluma mwenzao ambaye kwa hakika kuondoka kwake kumesababisha pengo kubwa katika Taaluma ya Uandishi wa Habari na Utangazaji hapa nchini.

“Kutokana na juhudi alizokuwa nazo Marehemu, Waandishi wa Habari na Watangazaji kote nchini hawana budi kuiga mfano wake na kuendeleza yote mazuri aliyoyafanya kwa maendeleo ya nchi yetu na Taifa letu kwa ujumla”, amemalizia Salamu zake za Rambirambi Rais Kikwete.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
21 Oktoba, 2013