Dk. Nchimbi Kufungua Mkutano wa Maofisa Waandamizi Jeshi la Magereza

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Emmanuel Nchimbi

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Emmanuel Nchimbi

Na Eliphace Marwa – MAELEZO

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Emmanuel Nchimbi anatarajia kufungua mkutano wa siku mbili wa Maofisa waandamizi wa Jeshi la Magereza utakaofanyika kuanzia Oktoba 24, mwaka huu mkoani Morogoro. Mkutano huo ndiyo mkutano wa juu kabisa katika Jeshi la Magereza ambao uwahusisha wakuu wa Magereza wa Mikoa ya kiutawala Nchini, Maafisa waandamizi toka Makao Makuu pamoja na Wakuu wa Taasisi sita za ndani ya jeshi la Magereza ambazo kimuundo wa utawala zina hadhi ya mikoa.

Taasisi hizo ni pamoja na Chuo cha maafisa Ukonga mkoani Dar es Salaam, Chuo cha mafunzo ya awali Kiwira Mkoani Mbeya, chuo cha Ufundi Ruanda Mbeya, chuo cha Udereva na ufundi mitambo cha Kingilwira mkoani morogoro, kikosi Maalum cha kutuliza ghasia Magerezani Ukonga Dar es Salaam pamoja na Shule ya Sekondari Bwawani iliyoko mkoani Pwani.

Aidha kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamishna  Jenerali wa Magereza Juma Mlewa inasema kuwa madhumuni ya mkutano huo wa kila mwaka ni kutathmini kwa pamoja utendaji wa jeshi hilo katika maeneo yake yote na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo pamoja na kurekebisha dosari zilizojitokeza na kuweka malengo ya kuboresha utendaji kazi katika mwaka unaofuata.

Mkutano huo, ambao mada kuu itakuwa ni utendaji kazi wa kasi na tija kwa matokeo makubwa sasa pia watazungumzia fursa mbalimbali za kuwezesha jeshi hilo kujitegemea, mpango wa uchangiaji wa hiari Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) pamoja na mada ya urekebishaji wafungwa itakayotolewa na Makao makuu ya Magereza. Mkutano huo unatarajiwa kufungwa na kamishna Jenerali wa Magereza John Minja.