Mbunge Chadema ataka muungano uvunjwe

Dodoma

MBUNGE wa Viti Maalumu, Mwanamrisho Abama (CHADEMA), ameiomba Serikali kuridhia Muungano uvunjwe. Abama alitoa kauli hiyo jana wakati akiuliza swali la kwa Waziri Mkuu, Abama alimnukuu Hayati, Abeid Karume ambaye aliufananisha muungano na koti.

“Kabla sijauliza swali langu nomba nimnukuu, Hayati Abeid Karume, alisema Muungano wetu ni kama koti, likikubana waweza kulivua mimi naona ni wakati muafaka wa kulivua koti hili.

…Muungano umekuwa na migogoro na malalamiko kutoka pande zote mbili, je serikali haiwezi kutia baraka zake ili muungano huu uvunjwe,” alihoji.

Abama alitaka pia serikali kupigisha kura za maoni baina ya pande mbili za muungano ili watoe maoni yao kama wanautaka muungano au hawautaki

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema pamoja na kwamba muungano umekuwa na matatizo lakini njia nzuri ni kukaa na kuangalia jinsi ya kuyatatua.

Yapo matatizo ya hapa pale katika muungano wetu, na miungano mingi duniani inafafana na sisi kwa matatizo kikubwa ni kuendelea kuzungumza ili kuuimarisha na kuongeza kuwa “Muungano wetu umetuletea heshima kubwa kama taifa”

“Lakini kwa sasa tupo katika mchakato wa katiba mpya, kama fikra zako hizi ndio fikra za wote basi tuziangalie katika katiba mpya.

…Rai yangu mimi ni kuendelea kuwa waangalifu kati suala hili la muungano, watanzania tupo zaidi ya milioni 44 na Zanzibar wapo milioni moja na kitu, muungano wowote utakaotaka kuziweka nchi hizi mbili katika mazingira yanayofanana itakuwa ni vigumu kuutekeleza.

…Ni vizuri kuwa na mfumo huu unaitambua Zanzibar pamoja na uchache wake wa watu

…Lakini mfumo huu wa kutaka kuwa na serikali ya Tanganyika , Zanzibar na Shirikisho matokeo yake yatakuwa sio mazuri lakini tupo huru kuchangia katiba yetu kwa jinsi tunavyoona inafaa,” alisema Pinda.

Katika hatua nyingine Bunge linatarajiwa kuwaka moto leo wakati Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, atakapokuwa akiwasilisha bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Ngeleja anawasilisha bajeti hiyo wakati watanzania wakikabiliwa na mgawo wa umeme ambao kwa kiasi kikubwa unaelezwa kushusha uchumi wa taifa kutokana na biashara nyingi kusimama baada ya kutokuwapo kwa nishati ya umeme wa uhakika.
Hata hivyo, jana wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo anayoulizwa Waziri Mkuu kila Alhamisi, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alitaka kujua ni kwa nini mgawo wa hauishi ingawa Serikali imekuwa ikitoa ahadi nyingi kwa ajili ya kukabiliana na hali hiyo.
Aidha Mbowe alitaka kujua ni kwa nini Ngeleja na Malima hawajajiuzulu nyadhifa zao licha ya kushindwa kukabiliana na kero hiyo.
“Kwa sababu taifa letu linakabiliwa na mgawo wa umeme ambao unatishia uchumi na ajira kwa wananchi na sasa Serikali imeonyesha haiwezi tena kutatua kero hii na wakati huo huo mawaziri husika bado wako madarakani na hawataki kujiuzulu, je unatoa kauli gani kuhusiana na hali hii?, aliuliza Mbowe.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisemo la umeme Serikali inalijua na iko katika mchakato wa kukabiliana nalo na kuliondoa kabisa.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Serikali imelazimika kubadili utegemezi wa umeme wa maji na kuangalia namna ya kutumia mafuta na gesi na pia jitihada zimefanyika kwa kuagiza majenereta nje ya nchi kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Hata hivyo jana hiyo hiyo, Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Lugola (CCM), aliomba mwongozo wa Spika na kueleza jinsi baadhi ya vyombo vya habari vilivyowahi kusema kuwa, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wamehongwa ili wapitishe bajeti ya wizara hiyo.
Kutokana na hali hiyo, alitaka uhakika wa taarifa hizo kwani siyo busara waziri kuwasilisha landama ya bajeti yake bungeni wakati kuna taarifa za wajumbe wa kamati husika kuhongwa.
Akijibu hoja hiyo, Spika Makinda alisema yeye binafsi hana taarifa za tukio hilo na akawataka wabunge kuchangia bajeti ya wizara hiyo kadili wanavyoweza na wasikubali kuhongwa.