Yohane Gervas Rombo
MKUU wa Wilaya ya Rombo, Elinasi Palangyo, amewataka wazazi na wadau wengine wa elimu wilayani hapa kuchangia jitihada zao ili kuinua na kuboresha elimu sambamba na kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa mpango wa sasa wa matokeo makubwa yaani ‘Big Result Now’.
Ameyasema hayo jana wakati alipokuwa akihutubia wazazi na wanafunzi katika mahafali ya kidato cha nne yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Mkuu.
Amesema kuwa serikali inajitahid kuboresha elimu na kukabiliana na changamoto hizo lakini akasema kuwa wazazi na wadau wengine pia wanayo fursa ya kusaidia kuinua na kuboresha elimu kwani suala hilo si la serikali peke yake.
Aidha mkuu huyo wa wilaya amewataka wanafunzi hao ambao wanatarajia kuhitimu kidato cha nne kutojiingiza katika matendo maovu kama vile matumizi ya dawa za kulevya pindi watakapokuwa nyumbani wakisubiri matokeo na badala yake watafute kitu ambacho wanaweza
kufanya ili wawe bize muda wote.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Wandiba amesema kuwa shule hiyo yenye wanafunzi elfu moja mia tatu na mbili.
Alisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa walimu hasa wa masomo ya sayansi na upungufu wa mabweni ya wavulana. Wandiba amesema kuwa uhaba wa walimu katika shule hiyo imekuwa ni changamoto kubwa hasa katika kipindi hiki ambapo wanatekeleza mpango wa matokeo makubwa sasa ‘BIG RESULT NOW’