HOTUBA YA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE SHEREHE YA KILELE CHA MBIO ZA MWENGE WA UHURU, KUMBUKUMBU YA BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE NA WIKI YA VIJANA KITAIFA
TAREHE 14/10/2013 MKOANI IRINGA
Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge;
Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo;
Mheshimiwa Zainab Mohamed, Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na watoto – Zanzibar;
Waheshimiwa Mawaziri na Nanaibu Mawaziri;
Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, Mkuu wa Mkoa wa Iringa;
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi;
Makamu Mwenyekiti wa CCM (wa Mkoa) na Viongozi wa Vyama vya Siasa mliopo;Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa Serikali wa Ngazi mbalimbali za Taifa na Mkoa;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Shukrani
Niruhusuni nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana tena mwaka huu kuadhimisha Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, kumbukumbu ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere na Wiki ya Vijana. Namshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Iringa, na viongozi wenzake pamoja na wananchi wa Iringa kwa kutupokea vizuri na ukarimu wenu. Pia nawapongeza kwa kukubali kuwa wenyeji wa maadhimisho haya. Kazi ya kuandaa sherehe kubwa kama hizi siyo jambo jepesi hata kidogo. Bahati nzuri mambo yamefana sana kama tunavyoshuhudia sote. Hongereni sana.
Pongezi Wizara
Ndugu wananchi;
Niruhusuni pia nitoe pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Mheshimiwa Zainab Omary, Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto wa Zanzibar kwa uongozi wao makini wa shughuli za Mbio za Mwenge. Kama tujuavyo shughuli za Mbio za Mwenge husimamiwa na Wizara zetu hizi mbili. Tunawapongeza kwa kazi nzuri waifanyayo. Ni ukweli ulio wazi kuwa kila mwaka tunashuhudia mambo yakiwa bora zaidi kuliko mwaka uliopita. Mcheza kwao hutunzwa. Hongereni sana.
Pamoja na Mawaziri napenda kuwatambua viongozi na wafanyakazi wote wa Wizara zetu mbili waliohusika na Mbio za Mwenge kwa kazi yao nzuri tunayojivunia sote. Aidha, nawapongeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya, viongozi na watumishi wa Serikali zetu mbili na wajumbe wote wa kamati mbalimbali walioshiriki katika kuratibu Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu. Wamefanya kazi nzuri inayostahili kupongezwa na kila mmoja wetu.
Kwa namna ya pekee nawapongeza ndugu Juma Ali Sumai, kiongozi wa Mbio za Mwenge na Wakimbiza Mwenge wenzake kwa kutimiza kwa ufanisi wa hali ya juu jukumu kubwa na zito la kukimbiza Mwenge wa Uhuru nchi nzima. Nawapa pole nyingi kwa changamoto mbalimbali walizokumbana nazo katika safari ya kilomita nyingi. Kazi hiyo wameimaliza salama na leo wameukabidhi Mwenge ukiwa salama. Nawapongeza sana kwa kuufikisha ujumbe wa Mwenge kwa uhodari mkubwa.
Waheshimiwa Mawaziri;
Ndugu wananchi;
Nafurahi kusikia kuwa kama ilivyokuwa miaka iliyopita, mwaka huu watu walijitokeza kwa wingi kila mahali Mwenge wa Uhuru ulipopita. Pia nimeambiwa ujumbe wa Mwenge ulifikishwa kwa ufasaha na kwamba umepokelewa vizuri. Miradi mingi ya maendeleo imezinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi.
Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa wananchi wa Tanzania kwa ushiriki wao mzuri katika Mbio za Mwenge. Ushiriki wao ni kielelezo tosha cha kutambua umuhimu wa Mwenge wa Uhuru na cha moyo wa uzalendo kwa nchi yetu na kuwaenzi waasisi wa taifa letu. Kwa niaba ya Serikali nawahakikishia kuwa tutaendelea kuwahimiza viongozi wa ngazi mbalimbali kuhakikisha kuwa miradi yote iliyozinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru inaendelea kutekelezwa kama ilivyokusudiwa.
Kwa namna ya pekee nawapongeza waandishi na vyombo vya habari kwa kuwa nasi bega kwa bega kuhamasisha watu na kueneza ujumbe wa Mwenge. Mchango wao umesaidia sana kufanikisha malengo ya Mbio za Mwenge kwani siku zote wapotoshaji hawakosekani.
Kumbukumbu ya Baba wa Taifa
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo siku ya kilele cha Mbio za Mwenge pia ni siku ya kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa letu la Tanzania kilichotokea miaka 14 iliyopita. Ni siku ambayo tunawajibika kukumbuka mema mengi aliyoifanyia nchi yetu, mafundisho yake na urithi aliotuachia. Nia yetu ni kutaka watu wasimsahau kiongozi wetu huyu maalum na muhimu sana katika historia ya nchi yetu.
Miongoni mwa mambo ya kukumbuka hasa wakati huu wa Mchakato wa Katiba Mpya ni (jambo la busara kutumia muda wetu) kujikumbusha mawazo ya Mwalimu kuhusu umoja wa nchi yetu pamoja na Muungano wa Zanzibar na Tanganyika. Hotuba zake na maandishi yake kuhusu mambo hayo yana mafundisho mengi mazuri ambayo tukiyaelewa vyema na kuyazingatia yatatusaidia sana katika mjadala na ukamilishaji wa mchakato wa Katiba mpya.
Mimi naamini fikra za Mwalimu na mtazamo wake kuhusu umoja wetu na Muungano bado vina maana hata leo. Tujiepushe na kuyapuuza tusije tukawa na Katiba itakayolibomoa taifa badala ya kulijenga. Ninaposema hivyo sipendi nieleweke kuwa sitaki mabadiliko ila napenda tuwe makini katika kufanya mabadiliko. Nataka tufanye mabadiliko yatakayotupeleka mbele na siyo kuturudisha nyuma.
Ndugu wananchi;
Pamoja na kuadhimisha siku ya kifo cha Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere), nadhani ni vyema pia tukawa tunaikumbuka siku ya kuzaliwa kwake yaani tarehe 13 Aprili (1922). Nisingependa kujiingiza katika mjadala wa siku ipi bora zaidi kwani zote ni siku muhimu katika historia ya maisha ya mwanadamu. Tofauti yake ni kuwa siku ya kuzaliwa ni ya furaha na siku ya kufa ni ya majonzi. Kama tutakubaliana tuikumbuke na siku yake ya kuzaliwa pengine siku hiyo tungeiita Nyerere Day. Tuiadhimishe siku hiyo kusheherekea maisha yake kwa kujadili kazi zake na kufanya shughuli mbalimbali kuenzi mambo mema aliyosimamia na kuifanyia nchi yetu na dunia kwa ujumla.
Kauli Mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2013
Ndugu Wananchi;
Kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri kila mwaka Mbio za Mwenge wa Uhuru huwa na ujumbe maalum unaobebwa na kauli mbiu ya mwaka huo. Mwaka huu ujumbe ulikuwa “Watanzania ni Wamoja: Tusigawanywe kwa Msingi wa Tofauti Zetu za Dini, Itikadi, Rangi na Rasilimali”. Ujumbe huu ni muafaka kabisa hasa ukikumbuka misukosuko na majaribu makubwa nchi yetu iliyopitia mwaka huu. Hivyo kutumia Mbio za Mwenge wa Uhuru kukumbushana haja na hoja za kuziba nyufa zilizoanza kujitokeza ni jambo la busara sana. Ni jambo la kuungwa mkono na kila mwananchi na hasa kila mzalendo.
Bahati nzuri upepo huo mbaya umepita na tuombe usirudi tena. Hivi sasa hali ni shwari na Watanzania tunaendelea kushirikiana vizuri bila ya kubaguana kwa dini zetu, vyama vya siasa na kadhalika kama tulivyozoea kuishi miaka yote. Waliotaka kutufarakanisha hawakufanikiwa lakini, lazima tuwe makini kwani wanaweza kujaribu tena kutugawa ama kwa yale yale au mambo mengine.
Ndugu wananchi;
Kwa kweli nafarijika sana kuona Watanzania wakiendelea kukataa ushawishi na uchochezi wa kugawanywa kwa misingi ya dini au mambo mengine. Ndugu zangu naomba tuendelee hivyo na hayo ndiyo mafundisho mema na urithi aliotuachia Baba wa Taifa tunayemkumbuka leo. Tukigawanyika, nchi yetu itavurugika na sote tutakuwa tumeharibikiwa. Dhambi kubwa ya kubaguana kwa misingi yo yote ile ni kupotea kwa amani na utulivu. Bila amani, hatuwezi kuishi kwa furaha katika nchi yetu hii nzuri. Bila amani, jamii haiwezi kujishughulisha kwa ukamilifu na shughuli za kujiletea maendeleo. Amani ikituponyoka nchi yetu itayumba na hakuna atakayebaki salama.
Napenda kuwahakikishia wananchi wenzangu wote, kuwa sisi Serikalini tutaendelea kufanya kila tuwezavyo kujenga, kulinda na kudumisha umoja na mshikamano wetu ambao ndio msingi mkuu wa kuwepo kwa amani na utulivu nchini. Tutaendelea kukemea kwa nguvu zetu na uwezo wetu wote vitendo vinavyosababisha mmomonyoko wa umoja na mshikamano wetu. Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu au kikundi cha watu watakaojihusisha na vitendo vya kuvuruga amani ya nchi yetu. Naomba Watanzania wenzangu mtuelewe hivyo. Napenda kusisitiza na kuwasihi kuwa tuendelee kuaminiana, kuheshimiana na kuvumiliana pamoja na tofauti zetu.
Mapambano Dhidi ya UKIMWI
Ndugu wananchi;
Pamoja na ujumbe huu maridhawa ambao kimsingi ndiyo ujumbe mkuu wa Mbio za Mwenge tangu kuasisiwa kwake, mwaka huu wananchi waliendelea kuhimizwa kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI, rushwa na dawa za kulevya. Tangu ugonjwa wa UKIMWI uingie nchini kwetu mwaka 1983, inakadiriwa kuwa zaidi ya ndugu zetu milioni 2 wamepoteza maisha kutokana na maradhi haya. Hali kadhalika zaidi ya watoto milioni 1.3 wamekuwa yatima na watu zaidi ya milioni 1.5 wanaishi na VVU hivi sasa. Bahati mbaya karibu asilimia 65 ya hao ni wanawake.
Kitaifa, takwimu zinaonesha kuwa maambukizi ya UKIMWI yanazidi kupungua kutoka asilimia saba mwaka 2005 hadi asilimia 5.7 mwaka 2010 na kufikia asilimia 5.1 mwaka 2012. Hapa Iringa napo maambukizi yamekuwa yanapungua ingawaje bado yapo juu na kwamba ni Mkoa wa pili nchini kuwa na kiwango cha juu cha maambukizi. Takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha maambukizi Mkoa wa Iringa ni asilimia 9.1, wanaume asilimia 6.9 na wanawake asilimia 10.9. Mkoa wa Njombe ndiyo unaoongoza ukiwa na asilimia 14.8.
Kwa sababu ya maradhi haya idadi ya watoto yatima ni kubwa katika mkoa huu (inakadiriwa kuwa waliopo ni 3400). Inahuzunisha sana kusikia au kuona baadhi ya watoto hawa wamelazimika kukatisha masomo yao baada ya wazazi wao kufariki ili kuwalea wadogo zao. Kwa ajili hiyo, wamelazimika kufanya kazi zisizostahili kufanywa na watu wa umri wao. Wapo pia wazee ambao kwa umri wao wanahitaji kulelewa lakini wamebaki peke yao na wakati mwingine wanalazimika kulea watoto walioachwa na watoto wao.
Ndugu wananchi;
Nilishaagiza viongozi siku za nyuma na leo narudia tena kuwa, tuwatambue watoto yatima kisha tutengeneze mipango thabiti ya kuwasaidia. Lengo letu hapa ni kutaka tuwawezesha kupata fursa ya kukua na kuishi kama watoto wengine. Jambo moja muhimu nililolisisitiza ni kuwa tuhakikishe kuwa vijana hawa wanapata elimu ambayo ndiyo ufunguo wa maisha yao.
Ndugu wananchi;
Tuongeze ari, nguvu na kasi ya kupambana na gonjwa hili hatari. Ni kweli tunapata mafanikio lakini hayatoshi. Kiwango bado ni cha juu mno. Nawaomba viongozi wa Serikali, dini, asasi za kijamii, wanasiasa na wananchi tuendelee kuhamasisha jamii kujiepusha na ugonjwa huu. Tuwahimize watu wajitokeze kupima wajue mustakabali wao, waepuke ngono nzembe na hasa hasa wawe na subira na waaminifu kwa ndoa zao au wapenzi wao. Sisi katika Serikali tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kuelimisha na kuhakikisha kuwa dawa za kufubaza vijijidudu vya UKIMWI zinapatikana bure kwa waathirika waliofikia hatua ya kutumia dawa hizo.
Natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa kuongeza juhudi maradufu kutokana na ukweli kwamba kiwango cha maambukizi kiko juu mno. Watu waendelee kujitokeza kwa wingi kupima kwa hiari ili kujua afya zao. Katika zoezi la kupima kwa hiari hapa Iringa, watu 388,071 wamejitokeza kupima. Jambo hili ni jema sana. Napenda pia kuchukua fursa hii kuwasihi akina mama wajawazito wawe mstari wa mbele kupima VVU ili wale walioathirika waitumie ipasavyo huduma ya kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Huduma hii inamfanya mtoto anayezaliwa na mama aliyeathirika kuwa salama. Huduma hii ipo kote nchini na inatolewa katika hospitali zote za Serikali.
Ndugu wananchi;
Ombi langu maalum kwa wanaume, kote nchini ambao bado hawajafanyiwa tohara wajitokeze kwa wingi kufanya hivyo. Madaktari wanasema kuwa mwanaume aliyefanyiwa tohara anapunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kuambukizwa VVU wakati wa kujamiiana. Naomba ieleweke kuwa sisemi mtu akifanyiwa tohara hapati UKIMWI. La hasha. Ninachosema ni kwamba ukimlinganisha na yule ambaye hakufanya hivyo, uwezekano wa kuambukizwa unapungua. Wanasema asiye na tohara ana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata michubuko ambayo hurahisisha virusi kuingia kwenye mwili wake. Narudia kusisitiza mtu akipata tohara asidhani yuko salama kabisa. Watu wote lazima wachukue tahadhari stahiki.
Ndugu wananchi;
Ombi langu la pili ni kwa watu wanaotumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI wasiache kuzitumia. Wakiacha kwa sababu yo yote ile wanavipa vijidudu nafasi kujiimarisha na hivyo kuhatarisha maisha yao. Ombi langu la tatu ni kwa jamii kuendelea kuwasaidia na kuwahudumia wenzetu ambao wameathirika badala ya kuwanyanyapaa na kuwatenga. Na, muhimu zaidi tuwasaidie watoto yatima na wazee ambao wameachwa bila msaada wowote.
Nawataka viongozi wote katika ngazi mbalimbali washiriki kwa ukamilifu katika mapambano dhidi ya maradhi ya UKIMWI. Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya na TACAIDS waendelee kuongoza mapambano hayo bila kuchoka. Mimi bado naamini Tanzania bila UKIMWI inawezekana iwapo tutazingatia masharti ya kuepuka ugonjwa huu na kuwahudumia ipasavyo walioathirika. Ushindi hauko mbali sana.
Mapambano dhidi ya Rushwa
Ndugu wananchi;
Mwaka huu, katika Mbio za Mwenge wa Uhuru wananchi waliendelea kukumbushwa wajibu wao katika kupambana na rushwa, kwa kauli mbiu isemayo “chukua hatua dhidi ya rushwa sasa”. Ujumbe huu unakwenda sambamba na juhudi za serikali za kupambana na rushwa nchini. Tunafahamu kuwa rushwa ni adui wa haki na kikwazo kikubwa cha maendeleo ya jamii na taifa. Nchi ikiwa imegubikwa na vitendo vya rushwa itakosa maendeleo stahiki na watu watadhulumiwa haki zao.
Hizo ndizo sababu kuu zilizoifanya serikali yetu ichukie rushwa na kuchukua hatua za kupambana na uovu huu, tangu nchi yetu ilipopata uhuru mpaka sasa. Kazi hiyo ngumu na yenye changamoto nyingi inaongozwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Serikali imechukua na itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha chombo hiki ili kiweze kutimiza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Matokeo yake TAKUKURU sasa ina mtandao mpana zaidi. Ina ofisi kila Mkoa na kila Wilaya, watumishi wameongezeka na vitendea kazi pia.
Nafurahi kuona kuwa mafanikio ya kutia moyo yanaendelea kupatikana ingawaje kazi iliyo mbele yetu bado ni kubwa. Sote tunasoma na kusikia kupitia vyombo vya habari taarifa za watumishi wa serikali, taasisi za umma pamoja na watu wengine wanavyokamatwa na TAKUKURU kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa. Tangu mwaka 2006, kesi 63 zinazohusu rushwa kubwa zimefikishwa Mahakamani. Baadhi zimeisha na wahusika waliopatikana na hatia wameadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Zipo pia tulizoshindwa, ni sawa katika nchi inayoheshimu utawala wa sheria. Nyingine zinaendelea. Vile vile juhudi za TAKUKURU zimeokoa fedha nyingi za umma. Kwa mfano, kwa kipindi cha miaka mitatu, yaani kati ya 2010 hadi 2013, zaidi ya shilingi bilioni 28 zimeokolewa ambazo zingeweza kunufaisha watu wachache wanaoendeleza vitendo vya rushwa badala ya taifa.
Naomba wananchi waendelee kutoa taarifa zitakazosaidia kuwatambua na kuwakamata watoaji na wapokeaji rushwa. Tukumbuke kuwa mafanikio katika mapambano haya hayategemei Serikali au TAKUKURU peke yake. Ni mapambano ambayo jamii ikijihusisha kwa ukamilifu ushindi mkubwa utapatikana. Yanatuhusu sote kwani tukishinda, matunda yake yatawafaidisha watu wote. Pia, napenda kutumia nafasi hii kutoa wito kwa taasisi na idara zote za serikali zinazohusika moja kwa moja katika vita dhidi ya rushwa zitimize ipasavyo wajibu wake. Aidha pakiwepo na ushirikiano mzuri na mshikamano wa dhati miongoni mwetu kwa hakika ushindi utapatikana. Tukifanya hivyo nina imani tutapata mafanikio makubwa zaidi tena kwa haraka.
Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Tatizo la biashara na matumzi ya dawa za kulevya limeendelea kuwa moja ya changamoto kubwa zinazolikabili taifa letu. Serikali imeendelea kufanya jitihada kubwa kupambana na changamoto hiyo. Yapo mafanikio yanayopatikana lakini bado tuna kazi kubwa ya kufanya mbele yetu. Ukubwa wa kazi hiyo unaletwa na ule ukweli kwamba watu wanaohusika ni wengi na wanazidi kuongezeka kila kukicha kwa tamaa ya kupata utajiri wa haraka. Isitoshe wakati wote washiriki wake wanabuni mbinu mpya za kusafirisha, kusambaza na kuuza dawa hizo haramu. Pia ni kazi hatari kwani wapambanaji kupoteza maisha si jambo la ajabu.
Pamoja na changamoto hizo, kwa vile matumizi ya dawa za kulevya yana athari mbaya kwa watu wanaotumia na jamii kwa ujumla, Serikali haitachoka kufanya kila tuwezalo kupambana na uhalifu huu mpaka ushindi upatikane. Wakibadili mbinu na sisi tutabadili maarifa ya uchunguzi na utambuzi mpaka tuwapate. Tutawahami ipasavyo watu wanaojitolea muhanga kupambana na uovu huu. Mafanikio yanaendelea kupatikana. Kwa mfano, kuanzia Januari hadi Septemba, mwaka huu (2013) watu 2000 (wafanya biashara na watumiaji wa dawa za kulevya) wamekamatwa na aina mbalimbali ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kilo 681 za dawa hatari ya heroine, zimekamatwa.
Watu hao kama wasingekamatwa wangeendelea kuuza na kusambaza dawa za kulevya na kuathiri maelfu ya watu na hasa vijana ambao ni nguvu kazi muhimu ya taifa letu na warithi wa jamii na taifa wa kesho. Inatia uchungu sana kuona kuwa tegemeo letu hilo linaangamizwa na watu wachache wenye uroho usio na kifani wa kujipatia utajiri wa haraka, tena kwa gharama yoyote ile.
Ndugu wananchi;
Kwa niaba yenu, napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa viongozi na wafanyakazi wote wa Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya na vyombo vingine vya dola kwa kazi kubwa na nzuri inayoendelea kufanyika ya kukabiliana na tatizo hili. Katika mapambano yetu tunashirikiana na nchi na taasisi za nchi mbalimbali duniani. Hivyo basi nazipongeza kwa dhati nchi na taasisi hizo rafiki kwa ushirikiano wao ambao umetusaidia kupata mafanikio haya kiasi tunayojivunia leo. Naomba ushirikiano huu uendelee kwani umetusaidia kwa namna nyingi na umekuwa wa manufaa makubwa.
Ndugu wananchi;
Nilishawahi kusema siku za nyuma kuwa ni makusudio yangu na ya serikali kuanzisha chombo chenye uwezo na nguvu kubwa zaidi ya kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini. Mchakato wa kuunda chombo hicho umeanza na unaendelea vizuri. Hivi sasa tunayo Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Chombo hicho kipya kitakuwa na nguvu kubwa zaidi kuliko Tume na hata kuliko kikosi kazi cha vyombo vyote vya dola nilichokiunda kuipa Tume meno.
Ndugu wananchi;
Ili juhudi hizo zifanikiwe na ushindi upatikane itategemea sana msaada, ushirikiano na ushiriki wa wananchi. Nawaomba sana ndugu zangu wananchi wenzangu mshirikiane na vyombo vya dola katika kupambana na usafirishaji, uuzaji na usambazaji wa dawa za kulevya. Baadhi yenu mnawajua watu wanaojihusisha na biashara hii haramu. Watajeni washughulikiwe ipasavyo.
Wiki ya Vijana
Ndugu wananchi;
Kama nilivyosema awali leo pia tunaadhimisha wiki ya vijana. Nimepata fursa ya kutembelea mabanda ya maonesho ya vijana ili kuona shughuli wanazozifanya. Nimefurahi na kufarijika sana na kile nilichokiona. Vijana wanafanya kazi nzuri na kwa kweli ni uamuzi wa busara kuwashirikisha katika sherehe hizi kwani wanapata fursa ya kuonesha kazi wanazozifanya katika kuboresha maisha yao na kuleta maendeleo ya taifa. Hii pia ni nafasi nzuri kwa vijana kukutana, kufahamiana na kubadilishana mawazo, ujuzi na taarifa muhimu zinazohusu maisha na maendeleo yao. Kwa kuzingatia umuhimu na faida ya maonesho haya, ni vyema kuangalia uwezekano wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana yakafanyika katika ngazi ya Mikoa na kuhitimishwa Kitaifa kama tulivyofanya leo.
Ndugu wananchi;
Mimi na wenzangu Serikalini tunatambua na kuthamini sana nafasi na mchango wa vijana katika kuchochea maendeleo ya nchi yetu. Ndio maana Serikali inawekeza sana katika elimu na mafunzo yao. Ndiyo maana pia Serikali imeamua katika mwaka huu wa fedha kuongeza uwezo wa bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ili iweze kuwahudumia vijana vizuri zaidi. Tutaendelea kuongeza bajeti hiyo ili Wizara iweze kuwaongezea vijana mitaji ya biashara kupitia Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana.
Nimefurahi kumsikia Mheshimiwa Waziri akiahidi hapa kwamba baadhi ya vijana walioshiriki katika maonesho niliyoyaona leo watafikiriwa kupewa mikopo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa. Nawasihi vijana watakaopata mikopo kupitia Mfuko huu pamoja na mifuko mingine ya uwezeshaji wahakikishe wanaitumia vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa na kuirejesha kwa wakati ili wengine nao wapate.
Maendeleo ya Mkoa wa Iringa
Ndugu wananchi;
Jana jioni nilipokea taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Iringa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Dokta Christine Ishengoma. Natoa pongezi nyingi kwa wananchi wa Iringa kwa juhudi zenu na mafanikio mnayoyapata katika kujiletea maendeleo. Mkoa umeendelea kuwa wa kutegemewa katika kulipatia taifa chakula hasa mahindi na sasa mwelekeo ni mzuri kwa mazao ya chai, mpunga, mboga na matunda. Nawaomba muendelee na juhudi zenu. Ongezeni maarifa na matumizi ya zana za kisasa na pembejeo za kilimo ili tija iongezeke mpate mavuno mengi zaidi. Mtatosheleza mahitaji yenu na mtapata ziada kubwa itakayotumika kwingineko nchini na hata kuuzwa nje ya nchi. Sisi katika Serikali tutaendelea kuwasaidia kwa upande wa upatikanaji wa pembejeo, zana za kilimo, masoko, huduma mbalimbali zikiwemo za ugani, fedha na kadhalika. Mkoa wa Iringa utanufaika kupitia Mpango wetu wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Result Now) na SAGCOT.
Ndugu wananchi;
Serikali itaendelea kununua mahindi ya wakulima kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Hata hivyo ni vyema nikaeleza wazi kuwa Hifadhi ya Taifa ya Chakula haitanunua mahindi yote yaliyovunwa nchini. Ukomo wetu kwa sasa ni tani 250,000 lakini tunaendelea kupanua uwezo wa maghala hadi kufikia tani 400,000 ifikapo mwaka 2015. Tayari Hifadhi ya Taifa wameshanunua tani 209,000 hivyo bado tani 41,000. Hivyo nashauri wenzetu wa sekta binafsi nao wajitokeze kununua mahindi ya wakulima.
Kwa kuwa hakuna kizuizi cha kuuza nje wanaweza kufanya hivyo wakipenda. Hata hivyo, sisi tungependa kwanza wauze hapa nchini. Naomba ieleweke kuwa hatutawauzia watu akiba yetu ya mahindi katika Hifadhi ya Taifa ya Chakula kwa ajili ya kuuza nje.
Ndugu wananchi;
Pamoja na kuendeleza kilimo katika Mkoa wa Iringa, tutaendelea kuboresha barabara, na huduma za umeme, maji, elimu na afya. Ninyi ni mashahidi kwamba utekelezaji wa ahadi ya kujenga barabara ya lami kutoka Iringa hadi Dodoma unakwenda vizuri na ukarabati wa barabara ya Morogoro – Tunduma kupitia Iringa na Mbeya umekamilika. Tunajipanga kutekeleza ahadi zetu kwa baadhi ya barabara za Mkoa huu.
Kwa upande wa umeme vijijini tunaendelea kuvipatia umeme vijiji 38 vya Mkoa huu na wakati huo huo tunajiandaa kuvipatia umeme vijiji vingine 86. Tutaendelea kuongeza upatikanaji wa maji vijijini na mijini. Aidha, tumeanza kutekeleza mkakati kabambe wa kuboresha elimu kwa shabaha ya kutoa fursa ya elimu kwa vijana wetu wengi na kuongeza kiwango cha ufaulu. Haya yote tunayafanya chini ya mkakati mpya wa kupata Matokeo Makubwa Sasa. Tutaongeza mara dufu juhudi za kuboresha huduma ya afya.
Hitimisho
Ndugu wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu niwakumbushe Watanzania wenzangu kuwa mwaka ujao ni wa aina yake katika nchi yetu. Kwanza tunasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, pili, tunasherehekea miaka 50 ya Muungano. Na tatu, kama mambo yatakwenda sawa tutapata Katiba Mpya. Niwaombe Watanzania wenzangu tujiandae vyema kufanikisha mambo yetu hayo matatu ya kihistoria. Naomba nimalize kwa kuwashukuru tena wananchi na viongozi wa Mkoa wa Iringa kwa kufanikisha sherehe hii muhimu. Nawashukuru pia wadau mbalimbali ambao wamechangia kwa hali na mali kufanya sherehe hizi zifanikiwe na kufana sana kama hivi. Napenda kutumia nafasi hii pia kuwatakiwa ndugu zetu Waislamu na Watanzania wenzangu wote heri ya Sikukuu ya Idd El Hajj.
Baada ya kusema hayo sasa natamka rasmi kwamba shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru, kumbukumbu ya Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Wiki ya Vijana kwa mwaka 2013 zimefikia kilele chake.
Asante sana kwa kunisikiliza.