WAZIRI MKUU Mizengo Pinda anaondoka Dar es Salaam Jumanne, Oktoba 15, 2013 kwenda China kwa ziara ya kikazi ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo inayotarajiwa kuanza Oktoba 16.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, lengo la ziara ya Waziri Mkuu ni kutangaza fursa za uwekezaji hapa nchini, fursa za biashara, za utalii na kutafuta mitaji kwa ajili ya sekta zilizo chini mpango wa matokeo makubwa ya haraka (Big Results Now Initiative).
Akiwa China, Waziri Mkuu atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Li Keqiang na viongozi wa Serikali ya China katika katika sekta za uchukuzi, mawasiliano, viwanda, madini na nishati.
Atatembelea mji wa Beijing na majimbo ya Shenzen, Chengdu na Guangzhou ambako atakutana na Makamu wa Rais wa China, Rais wa Benki ya Exim ya China, Rais wa Benki ya Maendeleo ya China, wakuu wa mashirika makubwa na kampuni kubwa nchini China na kufanya nao mazungumzo.
Waziri Mkuu Pinda ataungana na Wakuu wa Nchi watano kwenye ufunguzi wa maonyesho ya kibiashara ya magharibi mwa China (Western China International Fair – WCIF) ambako atahutubia washiriki wa maonyesho hayo. Pia atatembelea maeneo kadhaa ya uwekezaji na kufungua Kongamano la Uwekezaji baina ya Tanzania na China litakalofanyika Guangzhou.
Vilevile, Waziri Mkuu anatarajiwa kufungua mafunzo ya siku 10 kwa maafisa 20 kutoka idara na taasisi za serikali za hapa nchini yanayoendeshwa kwa pamoja baina ya Chuo cha Uongozi cha China na Taasisi ya Uongozi ya Tanzania. Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa Serikali kuboresha utendaji wa Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZ).
Waziri Mkuu ambaye anafuatana na Mawaziri wanne, wabunge wawili, wakuu wa mikoa watatu, wakuu wa taasisi wa Serikali na wawakilishi kutoka sekta binafsi, anatarajiwa kukutana na Watanzania waishia China huko Beijing na Guangzhou.
Tanzania imekuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu na China, nchi kubwa ya Bara la Asia, tangu mwaka 1964.
China yenye ukubwa wa kilometa za mraba 9,596,961 ina wakazi wapatao 1,349,585,838. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika Fedha la Kimataifa (IMF) nchi hiyo ni ya pili kwa uchumi mkubwa duniani.