Salma Kikwete Amtunuku Mtoto Ubalozi wa Heshima wa WAMA

MKE wa Rais Mama Salma Kikwete, na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)

MKE wa Rais Mama Salma Kikwete, na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)

Na Magreth Kinabo – MAELEZO
 
MKE wa Rais Mama Salma Kikwete, na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) amemtunuku Balozi wa kuwatetea watoto wa kike katika masuala ya elimu kutoka nchini Marekani, Califonia mwenye umri wa miaka (10) Zuriel Oduwole kuwa  mwanachama (balozi) wa heshima wa taasisi hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mama Kikwete mara baada ya Zuriel kuitembelea ofisi ya WAMA iliyoko Ikulu jijini Dares Salaam na kufanya mazungumzo kuhusu shughuli inazozifanya.

Mama Kikwete alimwezea Zuriel jinsi taasisi yake inavyofanya kazi  mbalimbali ikiwemo ya kuhakikisha watoto wa kike yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi wanapata elimu ili waweze kuajiriwa na kujiajiri ikiwa ni hatua ya kuendeleza maisha yao ya baade na kutimiza ndoto zao.

Kwa mujibu wa baba wa Zuriel, Ademola Oduwole alisema mtoto wake pia amekuwa akihamasisha wasichana kubadili mtazamo wa Bara la Afrika kwa kuwa huko Marekani watu hawalijuwi bara hilo na wanadhani ni bara la njaa. 

“Amezindua mradi wa dreaming up dreaming big’ lengo lake ni kuwahamasisha watoto wa kike kuwa na ndoto za kuendelea,” alisema  Oduwole.
 Oduwole aliongeza kuwa Zuriel anapenda kuhamasisha kuhusu suala la elimu kwa kuwa ndio njia ya kufikia malengo ya milinea. Alisema Zuriel ameshatembelea nchi Nigeria, Malawi na Tanzania ambapo alifika Shule ya Msingi ya Olympio na Shule ya Sekondari ya Jangwani na Shule ya Sekondari ya wasichana ya Marian. Pia ameshafanya mahojiano na marais wanane wa Afrika, ambao ni wa Tanzania, Mauritius, Kenya, Nigeria, Cape Verde, Sudan ya Kusini na Liberia.

Kwa upande wake Mama Kikwete alifurahishwa na juhudi za Zuriel na kumtaka kuendelea kufanya mambo makubwa katika kutimiza ndoto zake. Naye Zuriel alishukuru kwa ukarimu alioupata kwa Watanzania na ameaihidi kuitangaza Tanzania na WAMA mahali popote duniani.

Zuriel alikuwepo nchini kwa kipindi cha siku sita kuanzia Jumapili iliyopita akiwa na wazazi wake na wadogo zake Azaliah Arielle na Ismachiah, amerejea Marekani mwishoni mwa wiki hii.