Ikulu Tanzania Yatiliana Saini na UNDP Kuboresha Kilimo

Ikulu ya Tanzania

Ikulu ya Tanzania

OFISI ya Rais, Ikulu, na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Oktoba 7, 2013, zimetiliana saini mkataba ambako UNDP itaunga mkono jitihada za Serikali za kuanzisha Kitengo cha Kuharakisha Huduma za Kilimo (ADD) ndani ya Kitengo cha Rais cha Kuharakisha Huduma kwa Wananchi (Presidential Delivery Burea – (PDB).
Chini ya makubaliano hayo yaliyotiwa saini Ikulu, Dar Es Salaam, UNDP itaipatia PDB kiasi cha dola za Marekani milioni 9.5 ambazo zimetolewa kwa pamoja na Taasisi ya Bill and Melinda Gates ya Marekani na UNDP yenyewe.

Waliotia saini waraka wa makubaliano ambao unajulikana kama “Catalyzing Agricultural Developmenmt in Tanzania – Agricultural Delivery Division ni Katibu Mkuu Ikulu, Peter Ilomo kwa niaba ya Ofisi ya Rais, Ikulu na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bwana Alberic Kacou.

Fedha hizo zitatumika kutoa msaada wa kiufundi na kusaidia kuanzishwa kwa Kitengo kipya cha ADD.

Akizungumza kwenye hafla hiyo fupi, Bwana Kacou amesema kuwa chini ya makubaliano hayo, fedha hizo zitatumika kwa kipindi cha miaka mitatu na ameishukuru PDB, Ofisi ya Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uongozi wao ambao umewezesha UNDP, Bill and Melinda Gates Foundation, kuunga mkono jitihada hizo za Serikali.

Serikali ya Tanzania imeanzisha PDB kwa nia ya kuharakisha huduma kwa wananchi katika sekta sita muhimu kwa maendeleo ya wananchi.