Barrick yatoa bilioni 3.2l/- kwa mradi wa maji Shinyanga

KAMPUNI ya uwekezaji kwenye sekta ya madini ya African Barrick Gold (ABG) kupitia mgodi wake wa dhahabu wa Bulyanhulu uliopo wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, itawekeza dola za Marekani zisizopungua milioni 2 (sawa na shilingi 3.2 bilioni) kwenye mradi mkubwa wa maji ambao utawanufaisha maelfu ya wakazi wa eneo hilo.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Barrick imesema kuwa mradi huo utakapokamilika utawawezesha wakazi wa zaidi ya wilaya tatu kupata huduma ya maji safi na salama.

Meneja Mkuu wa mgodi wa Bulyanhulu, Kevin Moxham, alitia saini mkataba wa makubaliano wa mradi huo kabambe unaohusu ujenzi wa bomba jipya la maji tarehe 18 Mei mwaka huu.

“Mradi huu utahusisha ujenzi wa bomba la maji lenye urefu wa kilomita 60 ambalo litaunganishwa kwenye mtandao wa usambazaji wa maji unaoendeshwa na Mamlaka ya Maji Safi na Taka ya Kahama Shinyanga,” Barrick ilisema kwenye taarifa yake kwa umma.

“Bomba hilo jipya la maji litapita kwenye vijiji viliopo wilaya za Geita, Kahama na Shinyanga na litawapatia wakazi wa maeneo hayo maji safi na salama.”

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Bahati Mataka, amesema kuwa mradi huo mkubwa utakapo kamilika utaleta ufumbuzi wa kudumu wa tatito la muda mrefu la maji ambalo limekuwa likiwakabili maelfu ya wakazi wa wilaya hizo zinazopakana.

Hivi sasa wakazi wa vijiji viliopo karibu na mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu wamekuwa na shida ya maji kwa miaka mingi.

Hali hiyo imeifanya kampuni ya Barrick kuwekeza mabilioni ya shilingi kuhakikisha kuwa wakazi wa eneo hilo wanapata maji safi na salama.

Mgodi wa Bulyanhulu imeingia mkataba na halmashauri ya wilaya ya Kahama kwa niaba ya halmashauri za Geita na Shinyanga ambazo pia zitanufaika na mradi huo wa maji.

Ukosefu wa maji umekuwa ni tatizo kubwa linalozikabili wilaya hizo na kuwa ni chanzo cha matatizo ya afya kwenye eneo hilo.

Ingawa Barrick inatarajia kutumia dola za Marekani milioni 2 kwenye mradi huo, gharama kamili za mradi zitajulikana baada ya kufanyika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa ujezi wa mradi huo.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Bahati Mataka, amesema kuwa mradi huo utakapokamilika katika kipindi cha miaka mitatu, tatizo la miaka mingi la uhaba wa maji kwenye wilaya hizo litakuwa ni jambo la kihistoria.

Huu ni mradi wa pili mkubwa wa maji ambao mgodi wa Bulyanhulu umeufadhili baada ya kuwekeza mabilioni ya shilingi kwenye mradi wa kujenga bomba la maji kutoka Ziwa Victoria mpaka kata ya Bugarama ambapo mgodi wenyewe upo.