‘Wezesha Raia Kukabiliana na Tawala Sumbufu EAC’

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
 
Na Isaac Mwangi, EANA, Arusha

NCHI wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) hazina budi kutunga sheria inatakayowawezesha raia kuiwajibisha Serikali yoyote itakayokuwa “sumbufu” kwa watu wake, shirika la vyama vya kiraia vya kanda limesema.
 
Katika taarifa kali iliyotolewa na Jukwaa la Vyama vya Kiraia vya Afrika Mashariki (EACSOF) limeonya kwamba iwapo katiba haitazingatiwa, mazingira ya kazi ya kisheria na kisiasa yataendelea kuwa magumu zaidi.
 
“Kuna haja ya kutafuta katiba mpya kwa ajili ya Afrika Mashariki,” ilisema EACSOF katika taarifa yake iliyopatikana kwa Shirika Huru la Habari la Afrika Masharuiki (EANA).
 
Dalili za kudorora kwa mazingira muafaka kwa Afrika Mashariki, shirika hilo limesema ni pamoja na kutungwa kwa sheria mpya na kampeni mbalimbali za dola. Pia vipo vitendo vinavyolenga kudhibiti nguvu, haki na uhuru wa vyombo vya habari, vyama vya siasa, asasi za kiraia, wasomi na taasisi nyingine huru kama vile bunge na mahakama ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Kimataiafa ya Makosa ya Jinai (ICC).
 
“Zipo sheria mbaya zinazotoa nguvu kwa dola kufuta mashirika yasiyo ya kiseriklai (NGOs) yanayoonekana kuwa ni ‘sumbufu’ kwa serikali. Wakati katiba inawapa mamlaka raia kuiwajibisha vilivyo Serikali badala yake tunashuhudia kinyume cha matumizi mabaya ya uhusiano huo: wale ambao walitakiwa ”kuamriwa yaani serikali, badala yake wamegeuka kuwa makamanda.” Taarifa ilisema.
 
Kwa sababu mamlaka yamebaki kwa watu, taarifa hiyo imesema, wale ambao  mamlaka yao yamewekewa ukomo kikatiba yaani taasisi za serikali, hazitakiwa kisheria kufanya mabadiliko  au kuondoa mipaka hiyo kwa utashi wao.
 
“Kwa bahati mbaya katika nchi za kisasa za Kiafrika na hata nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uhusiano kati ya serikali na wananchi umekuwa ukigeuzwa juu chini. Sheria ni kitu kinachotengenezwa na serikali na siyo wananchi,” imefafanua taarifa hiyo.
 
Pia imeongeza kuwa; “utungaji wa sheria unajishughulisha zaidi na kulinda usalama wa nchi na maslahi ya utawala dhidi ya usalama wa binadamau, haki za msingi na uhuru.Sheria zinatungwa kukabiliana na matatizo ya muda mfupi, maslahi finyu na utunzi wa baadhi ya sheria ambazo ni kinyume cha maadili.”