Rais Kikwete Ahoji Umaskini Katika Dunia Tajiri, Ataka Afrika Kupata Kiti cha Kudumu UN

Rais wa Tanzania, jakaya Kikwete akihutubia Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York, Marekani.

Rais wa Tanzania, jakaya Kikwete akihutubia Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York, Marekani.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Septemba 27, 2013, amehutubia Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York, Marekani, na akataka kujua dunia inawezekana vipi kuruhusu kuendelea kuwepo umasikini katika dunia ambako kuna kila raslimali na uwezo wa kumaliza tatizo la umasikini.

Rais Kikwete pia amesema kuwa kama nchi tajiri duniani zingetoa fedha za kutosha, kama zilivyokuwa zimeahidi, ni dhahiri kuwa dunia ingeweza kufanikisha utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya Milenia (MDG’s) na malengo yake yote katika kipindi cha miaka 15 kama ilivyokuwa imeamuliwa mwaka 2000.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Afrika haitochoka kudai haki ya kufanyika kwa mageuzi ya msingi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) ili kuwezesha Bara hilo lenye idadi kubwa zaidi ya wanachama kwenye Umoja wa Mataifa (UN) kuwa na uwakilishi wa kudumu katika Baraza hilo.

Katika hotuba yake iliyoanza saa tisa za mchana (saa za New York) na kuchukua dakika 15 kamili, Rais Kikwete amesema ni jambo lisiloelezeka kuwa dunia ya leo inaendelea kushuhudia umasikini wakati kuna raslimali na utajiri wa kutosha wa kumaliza tatizo hilo kama upo utashi wa kutosha wa kisiasa na wa kutaka kumaliza tatizo hilo.

Rais Kikwete amekiambia Kikao hicho ambacho mada yake kuu ni Mjadala Kuhusu Ajenda ya Maendeleo Duniani Baada ya Mwaka 2015 – “Post-2015 Development Agenda: Setting the Stage” kuwa pamoja na kwamba umasikini mkali zaidi duniani umepunguzwa kwa nusu katika kipindi cha utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya Milenia (MDG’s) bado zaidi ya watu bilioni 1.2 wanaishi katika mtego mkubwa wa umasikini mkubwa.

Amesema kuwa mbali na watu hao, bado kiasi cha watoto wanaokadiriwa kufikia 19,000 chini ya umri wa miaka mitano na wanawake 800 hupoteza maisha yao kila siku kwa magonjwa ambayo yanaweza kabisa kuzuilika na kutibika na sababu nyingine zinazotokana na umasikini mkubwa.

“Hili ni jambo ambalo halikubaliki kabisa katika dunia iliyojaa neema ya kila aina tunamoishi leo ambako kuna maendeleo ambayo hayajapata kuonekana katika historia ya binadamu ya sayansi na teknolojia ambayo yanaweza kutumika kumaliza changamoto zote za maendeleo zinazokabili jamii ya binadamu sasa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Katika dunia ambako kuna chakula cha kutosha kumlisha kila mtu, hakuna sababu ya mtu yoyote kulala na njaa na kukabiliwa na ukosefu wa lishe. Katika dunia yenye utajiri mkubwa kama wa sasa, hakuna sababu kwa nini umasikini, njaa na dhiki viendelee kuleta dhiki na kusababisha shida kubwa kwa watu wengi kiasi hiki.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Katika hali hiyo, ni jambo lisiloingia akilini kwa nini Malengo ya MDG’s hayakufanikiwa kwa kiwango cha juu kabisa.”

Kuhusu kwa nini MDG’s hazikufanikiwa kwa kiasi kilichotarajiwa, Rais Kikwete amesema kuwa pamoja na changamoto zake ni dhahiri kuwa Malengo hayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

“Na kama nchi tajiri na zilizoendelea duniani zingekuwa zimetoa fedha na raslimali za kutosha kama ilivyokuwa imekubaliwa chini ya Lengo la Nane la MDG’s kwa mujibu wa makubaliano ya Monterrey na kwa mujibu wa ahadi zao katika mikutano ya nchi tajiri duniani ya G8 na G20, tungefanikiwa kutekeleza MDG’s zote za makubaliano yake ya mwanzo,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Kwa maana hiyo, litakuwa ni jambo la kujidanganya kama tulijadili nini tufanye kuhusu Malengo ya Maendeleo ya Milenia Baada ya 2015 bila kujadili na kukubaliana kuhusu jambo la msingi la jinsi ya kugharimia MDG’s hizi. Jambo hilo pia ni kweli kuhusu miaka miwili iliyobakia ya kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia.”

Kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama la UN, Rais Kikwete amesema kuwa hakuna tofauti za msingi za mawazo kuwa ni lazima yafanyike mageuzi ndani ya Baraza hilo. “Ukweli kuwa Umoja wa Mataifa unahitaji kufanyiwa mageuzi ni suala lenye tofauti kidogo. Kushindwa kwetu kwa pamoja kuchukua hatua za kukabiliana na ukweli huu unasababisha shaka kwenye shabaha yetu ya pamoja ya kuimarisha taasisi yenye lengo la kutumikia mataifa na watu wote duniani.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Mageuzi tunayodai yamechelewa mno. Wakati tunaendelea kudai mageuzi haya, Bara la Afrika halitachoka wala kupunguza kasi katika kudai mageuzi ndani ya Baraza la Usalama ili Bara hili, lenye idadi kubwa ya wanachama ndani ya UN, linapata sauti ya kudumu.

Mapema, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon na baadaye amekutana na kufanya mazungumzo na Wendy R Sherman, Waziri Mdogo wa Masuala ya Siasa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.