RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa pamoja na kwamba kiwango na maambukizi ya ugonjwa wa malaria yanapungua kwa kasi ya kuridhisha katika Tanzania, bado mtoto mmoja anapoteza maisha kwa ugonjwa wa malaria kila dakika moja katika Afrika. Aidha, Rais Kikwete ameishukuru Jumuia ya Kimataifa kwa juhudi kubwa za kupambana na ugonjwa wa malaria ambazo zimepelekea vifo kutokana na ugonjwa huo kushuka kwa asilimia 25 duniani na kwa asilimia 33 katika Afrika katika miaka 10 iliyopita.
“Ni jambo la kutia moyo kuwa dunia imefanikiwa kuzuia vifo vya watu 1.1 na kuondokana na kesi milioni 274 za malaria katika miaka 10 iliyopita.”
Pamoja na mafanikio hayo makubwa, bado Rais Kikwete amesema kuwa tishio la malaria bado ni kubwa ni kweli kwa sababu bado ugonjwa huo unasababisha vifo vya watu 650,000 kila mwaka.
“Changamoto yetu kubwa ni jinsi gani ya kudumisha mafanikio yaliyopatikana na kubakiza kasi ya sasa ya kukabiliana na malaria ili tupate mafanikio zaidi. Kwa sababu na kwa hakika, tishio la malaria bado ni kubwa, ni kweli na liko pale pale kwa sababu bado ugonjwa huo unasababisha vifo vya watu 650,000 kila mwaka,” amesema Rais Kikwete.
Rais alikuwa anazungumza kwenye Mkutano wa kuanzishwa kwa mpangokazi wa jinsi gani wadau mbali mbali wanaweza kushirikiana kupambana na ugonjwa malaria, mkutano ambao umefanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.
Rais Kikwete amewaambia wajumbe wa mkutano huo ulioandaliwa na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) na taasisi ya kimataifa ya Roll Back Malaria kuwa yamekuwepo maendeleo mazuri ya kupambana na ugonjwa wa malaria katika Tanzania na katika Afrika kwa jumla hata kama mapambano bado yanahitajika kupunguza zaidi athari za ugonjwa huo.
“Katika Tanzania vile vile tumefanikiwa kupata mafanikio ya kutia moyo ambako maambukizo ya ugonjwa huo miongoni mwa watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano yamepungua kwa nusu kutoka asilimia 18 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia tisa mwaka jana, 2012,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika Zanzibar, malaria imepungua mno na sasa tuko katika kipindi cha mpito kuelekea kwenye kumaliza kabisa tatizo hilo Tanzania Visiwani. Niruhusu nichukue nafasi hii kuwashukuru wadau wetu wa maendeleo kwa misaada yao iliyotufikisha hapo. Hata hivyo, nataka nitoa neno la onyo. Hii ni mara ya tatu, tunafanikiwa kumaliza malaria katika Zanzibar na inaweza kurejea tena. Hivyo, tunatakiwa kuwa macho kwa kuhakikisha kuwa malaria haisafirishwi kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar.”
Rais Kikwete amesema kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado balaa la malaria linatishia maisha ya watu bilioni 3.3 duniani na kuwa jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba watoto ndiyo wanaathirika zaidi. “Kwa hakika, kila dakika mtoto mmoja anapoteza maisha yake kwa ugonjwa wa malaria katika Afrika, Bara ambalo linabeba mzigo mkubwa zaidi wa ugonjwa wa malaria. Hali ni mbaya zaidi katika nchi za Afrika, Kusini mwa jangwa la Sahara, ambako asilimia 90 ya vifo vinavyotokana na malaria vinatokea.”
Rais Kikwete yuko katika ziara ya kikazi katika Marekani ambako atahudhuria na kuhutubia mkutano wa mwaka huu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN).
Rais Kikwete leo alikuwa miongoni mwa viongozi mbali mbali duniani ambao wamehudhuria kikao cha ufunguzi cha Baraza hilo ambacho kimehutubiwa miongoni mwa watu wengine ni Rais wa Brazil Mheshimiwa Dilma Rousseff na Rais Barack Obama wa Marekani.