VYOMBO vya ulinzi na usalama nchini Kenya vimefanikiwa kuokoa Jengo la Maduka ya Kisasa la Westgate lililovamiwa na wanaodhaniwa kuwa ni wanamgambo wa kikundi cha magaidi cha Al-Shabab. Kwa mujibu wa taarifa ambazo mtandao huu umezipata kutoka kituo cha Televisheni cha Citizen cha nchini Kenya, jengo hilo kwa sasa limeshikiliwa na vyombo vya usalama vya Kenya na kinachofanyika hivi sasa ni wanausalama kusafisha hatari yoyote inayoweza kujitokeza.
Jengo hilo la Ghorofa nne lilitekwa na kudi la magaidi wanaokadiriwa kufikia 10 na 15 tangu Jumamosi iliyopita tukio ambalo lilisababisha jumla ya raia wapatao 68 kupoteza maisha na wengine 175 kujeruhiwa. Taarifa zinasema magaidi wapatao 6 tayari wameuwawa katika tukio hilo la mapambano ilhali vyombo vya usalama vikifanikiwa kuokoa zaidi ya watu 1000.
Akizungumza na wanahabari kwa kifupi mara baada ya kuarifiwa vyombo vya ulinzi kudhibiti jengo hilo, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema taifa hilo linatoa shukrani kwa vyombo vya ulinzi na usalama, mashirika ya misaada, nchi anuai na wakenya walivyoshiriki kwa namna mbalimbali kuhakikisha wanaonesha umoja na nguvu katika kukabiliana na tukio hilo.
Alisema vyombo vya ulinzi kwa sasa vinaendelea na kazi ya uchunguzi wa tukio zima na kuhakikisha wote waliohusika wanapatikana na kuadhibiwa kikamilifu. “Hakuna watakao kimbia wote waliohusika ama kusaidia kutekelezwa kwa kitendo hicho tutawakamata na kuadhibiwa ipasavyo…,” alisema Kenyatta katika hotuba yake.
“Licha ya shughuli ya uokoaji jengo kukamilika bado inakadiriwa kuwepo kwa magaidi waliojificha ndani ya jengo hilo, hivyo vyombo vya usalama vinaendelea na zoezi la kusafisha eneo zima la tukio…,” alisema Kenyatta. Rais huyo ameahidi kutoa taarifa kamili hapo baadaye atakapolihutubia taifa baada ya kupata taarifa nzima kwa kina kwenye tukio hilo.
Wakati huo huo wabunge wa Bunge la Kenya katika kikao chao chaleo wamejadili tukio hilo na hali ya usalama kwa ujumla bungeni, huku wengi wakionekana kuitaka Serikali kuwekeza kiasi cha kutosha cha bajeti katika vikosi na idara za usalama wa nchi ili kuweza kukabiliana na matukio kama hayo. Wabunge hao wameonesha kuogopa hala ya usalama hasa la jengo lao na kushauri vyombo vya usalama kuwa macho zaidi kwani huenda sehemu inayofuata kuvamiwa ikawa ukumbi wa bunge hilo.
Tayari vyombo vya usalama vimefanikiwa kuwakamata watu kumi (10) huku wengine wakikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKIA ambao inasadikiwa huenda wanahusika katika tukio la uvamizi huo wa kigaidi, ulioitikisa Kenya kwa siku 4 mfululizo.