Mkurugenzi wa Uvinza Fm Ayubu Kalufya akitambulisha meza kuu kwa wageni waalikwa wakati wa hafla ya kuzindua
mradi wa UNESCO-UNDP wa kuhamasisha Amani katika mchakato wa kukuza Demokrasia katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mwaka 2015.
Mwenyekiti wa Bodi ya Uvinza Fm, Nuru Kalufya akiwasalimia wageni waalikwa kwenye uzinduzi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mwl. Khadija Nyembo akiteta jambo na Mtaalamu mhandisi wa mitambo na mafunzo ya awali kwa
watangazaji wa redio Uvinza Fm kutoka nchini Aurstralia Bw. Rukmin Wijemanne.
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma Mwl. Khadija Nyembo akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni
Kanali Mstaafu Issa Machibya wakati akizundua mradi wa UNESCO-UNDP wa kuhamasisha Amani katika mchakato wa kukuza Demokrasia katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mwaka 2015 uliofanyika kwenye Kituo tarajiwa cha Redio ya Jamii Uvinza Fm Wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
Sehemu ya wageni waalikwa na waandishi wa habari watarajiwa wa Redio Uvinza Fm wakimsikiliza mgeni rasmi.
Meneja wa Airtel mkoani Kigoma Philip Nkupama akizungumza nia yao ya kutoa ufadhili kwa Redio Uvinza Fm kurusha
matangazo yao kupitia minara ya Airtel ambapo pia amesema lengo lao ni kusaidia jamii zilizo na changamoto mbalimbali ikiwemo za mila potofu, Elimu duni, Ukeketwaji, imani za kishirikina, maendeleo duni, ukandamizaji wa Wanawake na Watoto na changamoto nyingine nyingi.
Ameongeza kuwa kupitia mradi wa Redio Jamii, Jamii itafikishiwa taarifa zote pamoja na kupambana na changamoto
mbalimbali nchini kwenye Siasa, Uchumi na Utamaduni na wakati huo huo kuiongezea jamii ufahamu kuhusu hali ya mwelekeo wa nchi yao kwa ujumla.
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mwl. Khadija Nyembo (wa tatu kushoto) akishiriki kucheza ngoma za asili na kinamama wa
Kikundi cha kinamama cha Uhamasishaji cha Warumba wilayani Uvinza.
Meneja wa Mradi wa Demokrasia na Amani kutoka Unesco Courtney Ivins akifafanua jinsi mradi huo utakavyotekelezwa na
Redio za Jamii nchini kuelekea uchaguzi mwaka 2015.
Kundi la Black and White kutoka wilayani Uvinza likitoa burudani ikiwa ni fundisho kwa mambo yanayojitokeza wilayani
humo lakini hayana mahali pa kusemewa, Redio Uvinza itasaidia kukomesha matukio kama hayo ya ukabaji.
Baadhi ya waandishi wa Redio Uvinza Fm wakisaidiana kubeba mitambo mipya ya Redio ya Jamii Uvinza Fm iliyotolewa na shirika la UNESCO kwa kushirikiana na UNDP.
Mtaalamu mhandisi wa mitambo na mafunzo ya awali kwa watangazaji wa redio Uvinza Fm Bw. Rukmin Wijemanne akihakiki mitambo ya Redio hiyo kama imekamilika tayari kuifunga. Kulia ni Meneja wa mradi wa DEP Courtney Ivins akikagua maboksi ya vifaa hivyo.
Mkufunzi wa Redio za Jamii kutoka Unesco Mama Rose Haji Mwalimu, Meneja wa Airtel mkoani Kigoma Philip Nkupama
wakiwa kwenye picha ya pamoja na waandishi na watangazaji watarajiwa wa Redio Uvinza Fm.
Na Mwandishi Wetu
Serikali inakaribisha miradi ya kuhamasisha amani katika mchakato wa kukuza demokrasia katika kipindi hiki cha
kuelekea uchaguzi mwaka 2015 inayozingatia habari za uhakika na maadili ya kiafrika kupitia radio za kijamii.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Bi Khadija Nyembo kwenye hafla ya
uzinduzi wa mradi wa shirika la umoja wa mataifa la elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO) wakishirikiana na shirika lingine la umoja wa mataifa la programu za maendeleo (UNDP) amesema mradi huu wa amani unahamasisha jamii umuhimu wa amani ili kukuza demokrasia nchini.
“mafunzo ya mafundi mitambo yanayoendeshwa na mtaalamu mhandisi wa mitambo kutoka Australia pamoja na mafunzo ya
awali kwa watangazaji wa redio kituoni hapa na wale maripota wa kujitolea kutoka baadhi ya vijiji na kata ambazo redio hii ya Uvinza FM itasikika, ni mafanikio makubwa kwa maendeleo ya wilaya ya Uvinza na mkoa wa Kigoma kwa ujumla,” amesema Kiongozi huyo.
Amesema wanahabari watakaoshiriki katika warsha hii ya siku tano watajifunza na kufanya mazoezi katika mada za kitaaluma pamoja na kanuni za maadili katika kutafuta na kuripoti habari.
“watajifunza habari ni nini, mbinu za kuibua habari, habari na jinsia na kuelimisha jamii. Watajifunza pia jinsi ya kuhariri habari, miundo mbalimbali ya vipindi kwa mujibu wa mwongozo mamlaka ya mawasiliano Tanzania-TCRA,’ amefafanua.
Bi Nyembo amesema Kampuni ya simu za viganjani ya Airtel imetoa msaada kwa kuruhusu minara yake itumike kurushia
matangazo kutoka kituo cha Uvinza FM Radio kwa upande mmoja na kwa upande mwingine wanashirikiana na serikali za mitaa katika kufanikisha mradi huo.
Amesema kitendo cha halmashauri ya wilaya ya Uvinza na halmashauri ya kijiji cha Uvinza kwa pamoja kutoa sehemu moja ya jengo la vijana kwa ajili ya Uvinza FM Radio ni jambo la kuigwa katika jamii kwa ujumla.
“Kwa niaba ya serikali yote hapa mkoani kwa ujumla natoa pongezi zangu za dhati kwa wadau hao wote waliowezesha na
watakaowezesha ukamilishaji wa mtambo huu na pia kuendeshwa kwa mradi huu wa UNESCO-UNDP wa uhamasishaji wa amani katika mchakato wa demokrasia kuelekea uchaguzi 2015.
“Kwa mujibu wa UNESCO mradi huu utazihusisha redio 26 zilizoko Tanzania bara na visiwani. Kati ya redio hizo tatu mpya zitajengwa na kuanzishwa Micheweni Pemba, Tumbatu Unguja ikiwemo Uvinza FM redio jamii Tanzania bara. Ni jambo la
kujivunia,”.