Tuwasaidie Wacongo, Wamechoshwa na Vita – Rais Kikwete

Rais Joseph Kabila (kushoto) akizungumza na Rais Kikwete

Rais Joseph Kabila (kushoto) akizungumza na Rais Kikwete


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Jumuia ya Kimataifa kufanya kila linalowezekana kumaliza mzozo wa kisiasa na mapigano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ili kutoa nafasi kwa wananchi wa Congo kuishi katika amani na kujitafutia maendeleo.

“Hawa ni watu walioteseka sana na kwa muda mrefu, wana haki ya kupata amani, wana haki ya kupata muda wa kupumzika kutokana na vita na mapigano,” Rais Kikwete ameuambia mkutano wa pili wa wakuu wa nchi zilizotia saini mkataba wa kutafuta amani, usalama na ushirikiano katika DRC chini ya Umoja wa Mataifa (UN).

Katika mkutano huo, uliofanyika Septemba 23, 2013, kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu wa UN, Mheshimiwa Ban Ki Moon kama ulivyokuwa mkutano wa kwanza uliofanyika Februari 24, mwaka huu, 2013, mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Kikwete amewaambia viongozi wenzake wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) na wengine waliotia saini mkataba huo:

“Nadhani hatua zilizochukuliwa mpaka sasa kuhusu DRC ni nzuri na mchakato wa kutafuta amani nchini humo unakwenda vizuri. Ni muhimu tukafikia mwisho wa tatizo hili kwa sababu wananchi wa DRC wametesema mno na kwa muda mrefu. Wana haki ya kupata amani, wana haki ya kupata muda wa kutosha wa kufanya mambo ya maana kama ya maendeleo yao badala ya kukaa na kufikiria vita,” Rais Kikwete amesema kwenye mkutano huo.

Rais Kikwete amesema kuwa siri ya kufanikiwa katika DRC ni kutekeleza yale yote ambayo nchi hizo zimekubaliana kutekeleza katika DRC akisisitiza: “La msingi ni kila mmoja wetu kutekeleza yale yote tuliyokubaliana. Hiyo ndiyo siri ya kuleta amani na utulivu katika DRC.”

Mbali na Rais Kikwete, mkutano huo wa leo umehudhuriwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye pia ni Mwenyekiti wa ICGLR, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Rais Joseph Kabila Kabange wa DRC, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Joyce Banda wa Malawi ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Mheshimiwa Nkosazana Dlamini-Zuma, na Katibu Mkuu wa UN ambaye alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo.

Aidha, mkutano huo umehudhuriwa na Makamu wa Rais na wawakilishi wa Jamhuri ya Congo (Congo-Brazzaville), Zambia, Angola na Sudan Kusini. Wenye mkutano huo, wasemaji wengi wamesisitiza kuwa hakuna amani ya kweli katika DRC na nchi za Maziwa Wakuu bila viongozi wa nchi hizo kukubali kuzungumza na kukubaliana na vikundi mbali mbali ambavyo vinapigana dhidi ya baadhi ya nchi hizo.

Baadaye leo, Rais Kikwete amehudhuria mkutano wa Baraza la Uongozi la Umoja wa Kutafuta Usalama wa Chakula na Ushirikiano wa Grow Africa uliofanyika kwenye Ofisi za Taasisi ya Uchumi Duniani (WEF) uliofanyika kwenye ofisi za taasisi hiyo katika Marekani mjini New York.

Rais alizungumza kwa ufupi katika mkutano huo ambako alitaka wafadhili wa miradi ya kilimo katika Afrika kuongeza kasi ya kutoa fedha za kuleta mageuzi ya kilimo katika Bara la Afrika kwa sababu kila mmoja wa wadau anatekeleza majukumu yake kwa haraka zaidi kuliko wafadhili