Kili yaandaa tamasha la Jivunie uTanzania


Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Bw. George Kavishe.

Na Mwandishi Wetu

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager imeandaa tamasha linalojulikana kama Kilimanjaro Premium Lager Fun Festival. Taarifa iliyotolewa jana Jijini Dar es Salaam na kusainiwa na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Bw. George Kavishe ilisema huu ni uzinduzi wa Kampeni ya Kili ‘Jivunie uTanzania’ kwa ajili ya kusherehekea Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania.

Bw. Kavishe alisema tamasha hilo pia linalenga kuwaleta pamoja mashabiki wa Simba na Yanga, watakaopata fursa ya kucheza mechi tofauti, ambapo washindi watapata zawadi mbalimbali zinazotolewa kwa udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager.

Simba na Yanga ndizo klabu vigogo zaidi hapa nchini Tanzania, ambazo pia hudhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager. Kwa mujibu wa meneja huyo, tamasha hilo litafanyika katika Viwanja vya Posta, Kijitonyama, Dar es Salaam Jumamosi ya Julai 16 mwaka huu na ni kwa ajili ya umma wote.

“Hili ni tamasha la mashabiki linalolenga kutangaza zaidi Kampeni yetu ya Jivunie uTanzania tuliyozindua kwa waandishi wa habari hivi karibuni kwenye Makumbusho ya Taifa,” alisema na kuongeza kwamba ushiriki wa kwenye michezo utakuwa wa hiari.

Alisema, “Zitatolewa zawadi nyingi wakati wa tamasha hili ambalo litakwenda sambamba na kanivali (carnival) ambayo ni aina ya sherehe itakayofanyika barabara nzima kuelekea Viwanja vya Posta ili kuwahamasisha Watanzania kujivunia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru,” akasema Kavishe.

Aliongeza kuwa tamasha hilo linatarajiwa kuanza mchana na kumalizika baadaye jioni. “Kutakuwa na bia nyingi aina ya Kilimanjaro na Nyama Choma ikienda sambamba nazo,” alisema meneja huyo.

TBL kupitia Kampeni ya Jivunie uTanzania, iliyozinduliwa kwa waandishi wa habari mapema mwezi huu, imeandaa shughuli mbalimbali zitakazoendelea hadi Desemba, wakati wa kilele cha Sherehe za Uhuru.