Eleuteri Mangi-Maelezo
WAMILIKI wa vyombo vya habari nchini wameaswa kuwajengea mazingira mazuri waandishi wa habari wa vyombo vyao ili waweze kuhabarisha umma wa Watanzania mambo mbalimbali yanayotokea ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia weledi wa taaluma yao.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake wa kuitumikia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Seith Kamuhanda leo alipokuwa anaagwa na watumishi wa wizara hiyo katika hafla iliyofanyika kwenye Uwanja wa Michezo wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“ Wamiliki wa vyombo vya habari wajenge mazingira mazuri ya kuwawezesha waandishi wa habari kusafiri ndani na hata nje ya nchi. Kwa kufanya hivyo unawapa fursa nzuri ya kujifunza mambo mengi ya kuihabarisha jamii ya Watanzania.
“Mwandishi asiye safari anakuwa na uelewa finyu wa mambo kwani ni jambo la msingi ajue nchi nyingine mambo yanaendaje ili aweze kulinganisha na maendeleo ya nchi yetu,” alisema Kamuhanda.
Kamuhanda alisema kuwa wamiliki wa vyombo vya habari kuwapa fursa waandishi wa habari kusafiri hilo ni jukumu lao la kwanza.
Kamuhanda aliongeza kuwa hata yeye alipokuwa mwandishi wa habari alijifunza mambo mengi alipokuwa akisafiri ndani na nje ya nchi, kwani kusafiri kunapanua mawazo na kuwa na uwezo mpana “exposure” wa kupambanua mambo juu ya nini cha kuandika na kuuhabarisha umma kulingana na maadili ya uandishi wa habari.
Aidha, Kamuhanda aliwaasa wamiliki na waadishi wa habari kuutumia vizuri uhuru wa vyombo vya habari uliopo hapa nchini. Sanjari na hilo, aliviasa vile vinavyokiuka miiko na maadili ya habari na kutumia vibaya uhuru huo vitambue kuwa wote wapo kwa ajili ya kuiletea sifa nzuri nchi yetu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa sasa wa Wizara hiyo, Sihaba Nkinga amempongeza Katibu Mkuu huyo aliyemaliza muda wake kwa kuitumikia Wizara hiyo kwa uaminifu kwa kipindi cha wa miaka minne.
Sihaba alisema kuwa Wizara anayoiongoza itaenzi kwa kusimamia na kuendeleza mambo aliyoanzisha Kamuhanda ikiwemo kudumisha umoja wa watumishi katika wizara na taasisi zake.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni Profesa Hermans Mwansoko akitoa neno la shukrani kwa Kamuhanda kwa niaba ya wafanyakazi alisema wizara hiyo itamkumbuka Kamuhanda kwa mpango wa kuwa na ofisi ya uhakika Dodoma, kuanzisha Bodi ya Filamu, kujali afya na uzima wa watumishi na kujali suala la jinsia katika ngazi za maamuzi ndani ya Wizara.
Kamuhanda alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na kufanya kazi chini ya Mawaziri George Mkuchika, Naibu wake Joel Bendera, Dkt. Emmanuel Nchimbi, Naibu wake Fenella Mkangara.
Hadi mabadiliko ya nafasi za makatibu wakuu yalipotokea hivi karibuni alifanya kazi chini ya Waziri Fenella Mkangara Naibu wake akiwa Amos Makala.