Rais Kikwete ashangazwa na uongozi wa wanasiasa

20130919-102446.jpg

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameshangazwa na kiwango cha uongo cha baadhi ya wanasiasa na hasa madai kuwa Rais aliteua wajumbe wa Tume ya Katiba bila kuongozwa na mapendekezo ya wadau mbali mbali waliopendekeza majina hayo.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa bado anaendelea kuamini kuwa mchakato wa Katiba Mpya utafikia mwisho wake mwakani, 2014, na hivyo kuiwezesha Tanzania kufanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 chini ya Katiba Mpya.

Vile vile, Rais Kikwete amesema kuwa hana tatizo na watu wanaopinga sera za Serikali ama hata kumpiga yeye binafsi bali tatizo lake ni wanasiasa na wanaharakati wanaochochea ghasia, fujo na uvunjifu wa amani.

Rais Kikwete aliyasema hayo juzi, Jumatatu, Septemba 16, 2013, mjini San Rafael, California wakati alipokutana na kuzungumza na Jumuia ya Watanzania waishio Jimbo la California, Marekani, wakati alipoanza ziara yake ya siku mbili katika Jimbo hilo ikiwa ni sehemu ya ziara ya Marekani.

Katika hotuba ambako alizungumzia mambo mbali mbali, Rais Kikwete aligusia mjadala wa karibuni Bungeni kuhusu mchakato wa Katiba Mpya na kusema kuwa alishangazwa na madai kuwa yeye kama Rais hakuongozwa na mapendekezo ya wadau wakati anateua Tume ya Katiba.

“Watu wote niliowateua walipendekezwa na wadau mbali mbali zikiwamo taasisi za dini. Yule Mama Maria Kashonda alipendekezwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Mama Mwantumu Malale alipendekeza Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA). Kila kundi ambalo lilipendekeza watu limepata mjumbe katika Tume hiyo wakiwemo walemavu ambao naambiwa nimewasahau,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Hivi nyie wanasiasa wenzangu mkikosa hoja mnaongopa hata kwa vitu ambavyo viko wazi kabisa. Tulikubaliana kuwa Rais angefanya uteuzi wa wajumbe wa Tume baada ya kupokea mapendekezo ya wadau mbali na katika mchakato ulioendeshwa kwa uwazi kabisa. Hivyo, ndiyo ilivyofanyika. Sasa uongo wa nini? Kama hakuna hoja ni kwamba hakuna tu na wala uongo hautasaidia.”

Kuhusu kama Tanzania itaweza kupata Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Rais Kikwete amesema: “Ningependa sana, na kwa kweli ni matarajio yangu makubwa, kuwa tuweze kumaliza mchakato wetu mwaka 2014 na tuweza kuwa na Katiba Mpya ili iongoze Uchaguzi Mkuu wetu wa mwaka 2015. Mchakato wetu unakwenda vizuri na wala siyo lazima tuhangaike na Katiba kwa miaka mingi. Muhimu ni ushirikishwaji wa kila mmojawetu.”

Akizungumzia tabia za wanasiasa wa Tanzania kwa jumla na hasa wale wanaochochea chuki na ghasia, Rais Kikwete aliwaambia Watanzania hao:

“Sina tatizo na wanasiasa ama wanaharakati kupinga Sera za Serikali yangu. Hili ni suala la nguvu ya hoja na tunao uwezo mkubwa sana wa kutetea Sera zetu. Na wala sina tatizo na watu kunipinga mimi binafsi. Kinachonipa taabu mimi ni pale wanasiasa na wanaharakati wanapochochea ghasia na kuleta fujo. Kama mtu anataka kuongoza Tanzania si asubiri hadi atakapochanguliwa?”

Aliongeza Rais Kikwete: “Hivi unapochochea ghasia, fujo na chuki na kweli mambo hayo yakatokea na nchi ikateketea, utaongoza nchi ya namna gani? Utaongoza magofu na majivu yatakayobakia baada ya nchi kuteketea?”

Kuhusu mjadala wa karibuni kuhusu kama Rais awe na madaraka ya kuteua wajumbe 166 wa nyongeza ili kuingia katika Bunge la Katiba kujadili Rasimu ya Katiba Mpya, Rais Kikwete amesema kuwa yeye hana taabu kama itabidi ateua basi atateua, lakini kama siyo lazima yeye hana taabu.

“Mimi sina taabu, wakisema niteua basi nitateua. Wakisema nisiteua vile vile sina taabu, isitoshe hiyo itakuwa inanipungumzia mzigo na kazi. Ile kazi yenyewe ya kuteua Wajumbe wa Tume ya Katiba ilikuwa siyo rahisi.”

Rais Kikwete alitumia siku ya pili ya ziara yake katika Jimbo la California kwa kutembelea Jiji la Vallejo ambako alikutana na Meya wa Mji huo, Mheshimiwa Osby Davis, pamoja na madiwani wa Jiji hilo na wafanyakazi wake.

Ziara hiyo ya Rais Kikwete katika Jiji laVallejo, nje ya Jiji la San Francisco, imekuja wakati wa Kumbukumbu ya Miaka 20 tokea Jiji hilo lianzishe uhusiano wa kidada na mji wa Bagamoyo ulioko Mkoa wa Pwani ulioanzishwa mwaka 1993.

Rais Kikwete alitumia muda mwingi wakati wa mkutano na baadaye wakati wa chakula cha mchana na viongozi wa Jiji hilo kujenga hoja ya kuvutia wawekezaji wa Jiji la Vallejo kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.

Rais Kikwete pia aliwaelezea viongozi wa Jiji hilo kuhusu historia ya Mji wa Bagamoyo na asili ya jina la mji huo lilitokana na enzi ya watumwa ambako mji uliitwa Bwaga Moyo (Tuliza Moyo Wako).

Rais Kikwete aliondoka mjini San Francisco usiku wa jana, Jumanne, Septemba 17, 2013 na amewasili mjini Washington, D.C. asubuhi ya leo kwa ajili ya ziara ya siku moja katika Mji Mkuu huo wa Marekani.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

18 Septemba, 2013