SISI, TGNP Mtandao, Haki Elimu, LHRC, Jukwaa la Katiba, TAMWA, Policy Forum na Mtandao wa Wanawake na Katiba, tukishirikiana na wana semina za jinsia na Maendeleo (GDSS) pamoja na wanajamii wa Tanzania tulioshiriki mjadala wa wazi kuhusu tunajifunza nini kutokana na mchakato wa Katiba mpya nchini Tanzania, leo tarehe 18 Septemba 2013 katika viwanja vya TGNP Mabibo DSM kwa lengo la kutafakari kuhusu mchakato wa Katiba nchini Tanzania ili kuainisha mafunzo makuu yatokanayo na mchakato huu kwa jamii ya Watanzania na fursa za maboresho ili kupata Katiba yenye muafaka wa wananchi tumebainisha na kujifunza yafuatayo:
1. Mchakato wa Katiba ni mchakato wa wananchi wote kwa sababu hiyo unajenga muafaka wa kitaifa na mchakato huu haukuanza bure ni madai ya wananchi.
2. Mchakato wa katiba unahitaji uelewa mpana wa wananchi, uhamasishaji, umiliki na ushiriki mpana ili kuwezesha katika utekelezaji wa kupata katiba mpya
3. Watanzania wanayo mawazo ya kisiasa, kiuchumi na kifalsafa kuhusu katiba hivyo basi tuwaachie wananchi waendelee na mchakato wa kupata katiba mpya
4. Mamlaka ya nchi yashushwe kwa wananchi ili waweze kushiriki na kufaidika na matunda ya taifa lao
5. Bunge la Katiba bado halina uwakilishi ulio sawa kwa wananchi wote hasa wanawake na wanaume walioko pembezoni
6. Tunahitaji kuweka tofauti zetu pembeni na kuwa na mshikamano, sauti moja na nguvu za pamoja ili kupata katiba yenye misingi ya demokrasia
Sisi wanaharakati wa mashirika yaliyotajwa hapo juu tunadai yafuatayo:
i) Muswada wa Sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba 2013 irudi kwa wananchi ili uweze kujadiliwa na kupata maoni ya watanzania walio wengi kwani katiba ni mali ya wananchi wote na kupitisha muswada huu bila kushirikisha makundi yote kutaendeleza mifumo kandamizi hasa kwa wanawake na wanaume walioko pembezoni.
ii) Mchakato wa kupata katiba mpya usifanywe kuwa ni siasa na tuache mara moja kuchanganya siasa na mchakato huu pia usiharakishwe
iii) Mchakato wa kutunga sheria ya kura za maoni uwe shirikishi na maoni ya wananchi yazingatiwe
iv) Wananchi waachiwe wasimamie mchakato wa katiba ili masuala ya msingi yanayowagusa kama vile maji, afya, elimu na ardhi yaweze kubebwa.
Limetayarishwa na kusainiwa na:
1. TGNP Mtandao …………………………………………..
2. LHRC ……………………………………………
3. Policy Forum ……………………………………………
4. WFT …………………………………………….
5. Hali Elimu …………………………………………….
6. Jukwaa la Katiba …………………………………………….
7. TAMWA ………………………………………………