Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka Watanzania kuisemea, kuijenga na kuitetea nchi yao badala ya kushiriki katika kuikejeli na kuidharaulisha.
Rais Kikwete amesema kuwa kuisemea na kuitetea Tanzania ni wajibu wa kila Mtanzania awe anaishi ndani ya nchi ana ughaibuni.
Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la ajabu kuwa kazi ya kuisemea, kuitetea na kujenga jina zuri la Tanzania inafanywa zaidi na watu wa nje kuliko baadhi ya Watanzania na hasa wale wanaoishi nje ya nchi.
Rais Kikwete ameyasema hayo usiku wa jana, Jumatatu, Septemba 16, 2013, wakati alipokutana na kuzungumza na Watanzania waishio katika Jimbo la California kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili katikia jimbo hilo na baadaye katika sehemu nyingine za Marekani.
Rais Kikwete amewaambia Jumuia ya Watanzania katika Hoteli ya Embassy, San Rafael, California: “Ni wajibu wa Watanzania popote walipo kuisemea vizuri na kutetea maslahi ya nchi yao. Ni jambo lisilo na tija kushiriki katika kuilaumu na kuikejeli nchi yetu. Utasikia na kusoma kwenye mablog baadhi ya watu wakisema kuwa ‘hii nchi gani?” amesema Rais Kikwete.
Rais ameongeza: “Siyo tu kwamba ni wajibu wa kila mmoja wetu kuisemea Tanzania lakini ni wajibu wetu kusaidia kusukuma maendeleo ya Tanzania. Hakuna mtu mwingine wa kuifanya kazi hii isipokuwa Watanzania. Hii ndiyo nchi yetu. Hakuna nchi nyingine hata kama tunailaumu kiasi gani.”
Amesisitiza: “Kama watu wa nje wako tayari kuisemea nchi yetu, nyie mnashindwaji vipi kuifanya kazi hiyo ya kuitetea nchi nzuri hii? Hivi nani tunamwachia aijenge nchi hii, aitetea nchi hii? Wengine wanathubutu kuuliza ‘Nchi nzuri? Turudi’. Hivi nani ulimwachia akujengee nchi nzuri ili uweze kurudi?”
Rais Kikwete amesema kuwa ni lazima Watanzania wajifunze kutoka kwa wenzao, wakiwemo majirani zao kuhusu namna ya kutetea maslahi ya nchi yao kwa kila jitihada.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
17 Septemba, 2013