Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake haitawatetea Watanzania wanaokamatwa wamebeba dawa za kulevya nje ya nchi kwa sababu biashara ya dawa hizo ni haramu na uvunjaji wa sheria katika Tanzania pia.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake haina uhakika kama suala la uraia pacha (dual citizenship) litaweza kuwemo katika Katiba Mpya kwa sababu suala hilo halikuwamo katika Rasimu ya Katiba hata kama limependekezwa tena na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Vile vile Rais Kikwete amesema kuwa ni wajibu wa Watanzania wanaoishi ughaibuni kuwa raia wema na kufuata na kuheshimu sheria katika nchi wanamoishi kwa sababu wakivunja sheria za nchi hizo Serikali yake haitawatetea.
Rais Kikwete ametoa ufafanuzi huo usiku wa jana, Jumatatu, Septemba 16, 2013, wakati alipokutana na kuzungumza na Watanzania wanaoishi katika Jimbo la California, Marekani, kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili katika Jimbo hilo. Rais Kikwete amewasili mjini San Francisco, California mchana wa jana kuanza ziara hiyo.
Akizungumza na Watanzania hao katika Hoteli Embassy iliyoko San Rafael, Rais Kikwete amesema kuwa ni kweli kuwa Watanzania wamejiingiza kwa kiasi kikubwa katika kufanya biashara ya ovyo ovyo kama ile ya dawa za kulevya lakini kuwa Serikali yake haitawatetea Watanzania wanaokamatwa wakishiriki biashara hiyo.
“Ukikamatwa na dawa za kulevya hatukutetei kwa sababu hata sheria za nchi zetu zinazuia biashara hiyo. Sisi hatuwezi kuendelea kuwa na sifa ya kufanya biashara za ovyo ovyo kiasi hicho. Serikali itawatetea Watanzania wanaoishi nchi za nje ikiwa wataonewa. Lakini ukifanya biashara ya madawa ya kulevya ama kubaka watu hatukutetei kamwe,” amesema Rais Kikwete.
Kuhusu suala la uraia pacha kuwekwa katika Katibu Mpya, Rais Kikwete amesema kuwa katika maoni ya awali suala hilo halikusikika kiasi cha Wajumbe wa Tume ya Katiba kuliweka katika Rasimu ya Katiba.
“Lakini sisi katika CCM tumelizungumza na kuliweka katika mapendekezo yetu mapya tulipokaa kama Baraza la Katiba. Tunataka lizungumzwe. Hatuna hakika kama litawekwa katika Rasimu ijayo, lakini tutaendelea kulisemea. Kubwa ni kwamba hili ni jambo ambalo halitapata sauti za kutosha kulisemea. Lakini faida zake zinaeleweka hata kama inaelekea kuwa hakuna watu wengi wanaokereketwa na jambo hili kiasi cha kulisema kiasi cha kutosha katika mjadala wa Katiba.”
Rais Kikwete pia amewashauri Watanzania wanaoishi nchi za nje kuishi kwa amani, kuheshimu sheria na kutojiingiza katika mambo yanayoweza kuwaingiza katika matatizo.
“Lazima muwe raia wema. Mliamua wenyewe kuja kuishi katika nchi hizi. Nchi hizi zina sheria zake. Kama mtaamua kuwa raia wabaya wanaovunja sheria mtaingia katika matatizo – kama wasemavyo Waingereza you will face the music and sometimes that music may not be enjoyable.”
Kuhusu ombi la Watanzania waishio nje za nje kuruhusiwa kupiga kura, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake haina tatizo wala pingamizi ya suala hilo ili mradi tu Tume ya Uchaguzi ya Taifa iwe na uwezo wa kulifanikisha jambo hilo. “Kama wanaweza hakuna pingamizi. Hatuna matatizo na jambo hili.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
17 Septemba, 2013