WAFANYABIASHARA WA MAHINDI katika mji mdogo wa Himo, uliopo km 10 kutoka kituo cha Holili, mpakani mwa Kenya na Tanzania mkoani Kilimanjaro, wanasema Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imekuwa tishio zaidi kuliko kuwa msaada katika biashara yao.
‘’EAC haitusaidii.Imeleta uhuru usiodhitiwa kwa wenzetu wa Kenya kwenda na kununua mahindi moja kwa moja kwa wakulima na kusafirisha kupeleka Kenya.Hali hii inatishia uhai wa biashara yetu,’’ alisema mfanyabishara wa nafaka katika mji mdogo wa Himo, Modest Merkior.
Akizungumza na Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA),Merkior alisema katika hali ya kawaida wafanyabiashara kutoka nchi jirani ya Kenya wangeweza kununua mahindi na nafaka nyingine Himo ambako ndiko soko lilipo.Lakini hili sasa halipo, wanadai na hivyo kuwafanya wakose biashara hiyo.
EANA, kwa kushirikiana na Asasi ya Vision East Africa (VEAF), ambalo ni jopo la wataalamu wa kanda,wanafanya utafiti katika vituo vya mipakani vya EAC kubaini kiwango cha uelewa wa raia juu ya jumuiya na manufaa yake. Utafiti huo unafadhiliwa na Shirika la Misaada la Ujerumani (FES), ofisi ya Tanzania.
Wafanyabiashara wengine wa mahindi na wamiliki wa maghala ya kutunzia nafaka katika eneo hilo pia, Samwel James na Chenono Herman,waliounga mkono hoja hiyo.
Walitoa wito kwa serikali ya Tanzania kuchukua hatua za makusudi ya kuweka sera ya kuwapendelea wazawa na kuwalinda kutokana na kile walichokiita ‘’mazingira yasiyosawa ya biashara.’’
‘’Uhuru huu lazima udhibitiwe. Wafanyabiashara hawana budi kuja Himo au katika eneo lililotengwa maalum kwa soko la mahindi.Huwezi kufanya hivyo nchini Kenya,’’ James alilalamika kwa uchungu.
Alisema iwapo zipo sababu za msingi za kuruhusu wageni kwenda maeneo ya ndani kununua mahindi na nafaka nyingine, basi mfanyabiashara wa aina hiyo hana budi kusindikizwa na mtanzania.
Mfanyabiashara mwingine Amos Masiga, aliongeza kwamba taasisi za fedha na mabenki haziwaungi mkono kwa kuwapatia huduma ya mikopo.
‘’Kwa nini mabenki kama NBC (Benki ya Taifa ya Biashara), Benki ya CRDB na nyinginezo haziji kutuelimisha ili kutupatia mikopo kwa biashara hii? Kwa nini hujifungia katika ofisi zao wenyewe badala ya kuja kwetu? Ningekuwa na uwezo kifedha,bila shaka ningeweza kuboresha biashara yangu,’’ alilalamika.
Masiga alitoa wito kwa taasisi za fedha ikiwa ni pamoja na mabenki kufanya juhudi za kuwatafuta walipo ili kuwapatia huduma za mikopo ya benki kwa ajili ya biashara zao.
Wafanyabiashara wa Kenya, wake kwa waume wanadaiwa kuwa huru kuingia Tanzania kununua mahindi, mchele,maharage na vitunguu katika maeneo mbalimbali kama vile Kiteto, Mbulu na Babati katika mkoa wa Manyara na katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.