Rais Kikwete Ziarani Marekani na Canada

Ndege ya Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini Septemba 15, 2013, kwenda Marekani na Canada kwa ziara za kikazi ambako miongoni mwa shughuli zake nyingine nyingi atahutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York.

Ziara ya Rais Kikwete itaanzia katika Jiji la San Francisco, Jimbo la California, ambako atakuwa na ziara ya siku mbili na ambako atafungua Ubalozi Mdogo wa Tanzania katika jimbo hilo kubwa zaidi kuliko mengine katika Marekani na pia kukutana na Jumuia ya Watanzania waishio katika Jimbo hilo. Rais pia atakutana na kufanya mazungumzo na Meya Osby Davis wa Mji wa Vallejo.

Jumatano, Rais Kikwete atakuwa mjini Washington, D.C., kwa siku moja ambako atakutana na viongozi wa Bunge la Marekani kwa chakula cha mchana, atahudhuria sherehe ya kutiwa saini kwa mikataba ya kufunguliwa kwa Balozi Ndogo za kuwakilisha Tanzania katika sehemu mbali mbali za Marekani na pia atahudhuria dhifa ya mwaka ya Kamati Ndogo ya Bunge la Marekani kuhusu hifadhi za wanyama na ardhi.

Alhamisi, Rais Kikwete atakwenda mjini Toronto, Canada ambako siku ya pili atatunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu (PHD) ya Sheria na Chuo Kikuu cha Guelph.

Baada ya hapo, Rais Kikwete atarejea tena katika Marekani zamu hii mjini New York ambako atakuwa na shughuli nyingi akianza na kuhudhuria halfa ya taasisi ya kupambana na ugonjwa wa malaria duniani ya Roll Back Malaria, na baadaye kuhudhuria shughuli ya namna ya kuongeza kiwango cha Lishe duniani. Aidha, Rais Kikwete atahudhuria Mkutano wa Nchi Wanachama wa Maziwa Makuu na pia kukutana kwa mazungumzo na Rais Alassane Quattara wa Cote d’Ivore.

Vile vile akiwa mjini New York, Rais Kikwete atahudhuria halfa rasmi itakayoandaliwa na Rais Barack Obama wa Marekani kwa ajili ya viongozi mbali mbali duniani na Jumanne ijayo asubuhi atahudhuria ufunguzi wa Kikao cha 66 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambacho kitahutubiwa na Katibu Mkuu wa Umoja huo, Mheshimiwa Ban Ki Moon na baadaye kuhudhuria Chakula cha Mchana ambacho kitaandaliwa na Katibu Mkuu huyo kwa ajili ya viongozi mbali mbali duniani wanaohudhuria Kikao hicho.

Rais pia atakutana kwa mazungumzo na Daniel Yohannes, Mtendaji Mkuu wa Millennium Challenge Corporation (MCC), inayogharimia miradi ya mabilioni ya fedha katika sekta ya miundombinu katika Tanzania, atakutana kwa mazungumzo na Katibu Mkuu Ban Ki Moon, atahudhuria Mkutano wa Mwaka wa Taasisi ya Clinton Global Foundation ambayo inagharimia miradi mbali mbali katika Tanzania.

Rais Kikwete atahutubia Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa saa tisa mchana (saa za Marekani) Septemba 26, mwaka huu, 2013 ambako atazungumzia Ajenda ya Maendeleo Duniani baada ya mwaka 2015.