Afrika Mashariki: Kutojua Kiingereza Kikwazo cha Biashara
Na Mtuwa Salira, Arusha
WAFANYABIASHARA wa nafaka katika mji mdogo wa Holili, Kaskazini mwa Tanzania, mpakani na Kenya wamesema kutojua lugha ya Kiingereza kwa ufasaha ni kikwazo katika ufanyaji biashara mipakani.
“Lugha ya Kiingereza inatutesa. Lazima tuchukue hatua kuboresha ujuzi wetu wa lugha ya kigeni kama kweli tunataka kushindana kufanyabiashara ipasavyo na wenzetu,” Samwel James, mfanyabiashara wa mahindi na mmiliki wa ghala la nafaka Himo aliliambia Shirika la Habari Huru la Afrika Mashariki (EANA).
EANA, kwa kushirikiana na Asasi ya Vision East Africa (VEAF), ambalo ni jopo la wataalamu wa kanda, wanafanya utafiti katika vituo vya mipakani vya EAC kubaini kiwango cha uelewa wa raia juu ya jumuiya na manufaa yake. Utafiti huo unafadhiliwa na Shirika la Misaada la Ujerumani (FES), ofisi ya Tanzania.
James alisema uelewa mzuri wa lugha ya Kiingereza ungemweka katika hali bora zaidi ya kufikia mikataba ya biashara na kuwashawishi wateja toka nje kununua bidhaa zake.
“Nilikwenda Malawi na rafiki yangu kwa shughuli za kibiashara lakini hatukuweza kuzungumza moja kwa moja na maofisa wa serikali mpakani wala kuzungumza kwa uhuru na wafanyabiashara wenzetu. Tulilazimika kumkodi mkalimani,” alisema Amos Masiga, mfanyabiashara wa mahindi Himo.
Masiga alisema nchini Malawi, wenyeji wanaweza kuzungumza lugha za makabila yao kama vile Kichewa lakini pia huzungumza vizuri Kiingereza. “Kwa nini sisi tusifanye kama wao, yaani kuzungumza lugha zote Kiswahili na Kiingereza?”
Alisema hakuna upinzani kwamba Kiswahili kiendelee kuwa lugha ya taifa, lakini kwa kuwa lugha ya Kiingereza inazungumzwa katika kanda na duniani kote, ni muhimu kujifunza kwa sababu ya mawasiliano na biashara.
Naye Diwani wa Kata ya Holili, wilaya ya Rombo, Onesmo Myombo aliunga mkono maoni ya wafanyabiashara hao.
“Hatuna lugha ya biashara ambayo ni tofauti na ile ya jirani zetu wa Uganda na Kenya. Lakini wenzetu wanatangaza zaidi biashara ya utalii na nyingine kwa sabau tu ya kufahamu lugha ya Kiingereza vizuri,” alisema.