Na Anna Nkinda – Maelezo
WAUMINI wa dini ya Kiislam nchini wametakiwa kuwa pamoja katika kuendeleza masuala ya kiimani bila ya kuhitilafiana kwani hititafu ndogo huzaa migogoro katika jamii jambo ambalo linaweza kusababisha kuvurugika kwa amani iliyopo.
Wito huo umetolea jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa ufunguzi wa msikiti na madrasa wa Masjid Madinatil Munawwar uliopo Kibingu – Msanga Zalala kijiji cha Msimbu wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema viongozi wa dini wanayo kazi kubwa ya kuwasomesha na kuwaelimisha vijana wa Kiislam katika kumcha Mwenyezi Mungu na kuwaasa juu ya kulinda amani iliyopo kwaajili ya maisha yao na watu wengine.
“Naomba niwausie juu ya jambo hili kwani sisi wote ni waislamu ambao tunaongozwa na kitabu kimoja na tunaabudu katika njia moja tusitumie muda mwingi kuwa na marumbano kwenye misikiti yetu kuhusu imani.
Lakini pia tusiwe chanzo cha misuguano ambayo inaweza kuhatarisha amani ya nchi bali tuwe na subira na kuvumiliana kama kuna tofauti yoyote baina yenu mkae kwa pamoja na kutatua tatizo lililopo”, alitoa wosia Mama Kikwete
Aidha Mama Kikwete pia aliwataka waumini hao kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata elimu ya dini na Dunia ili waweze kuwajengea msingi bora wa maisha yao ya baadaye kwani watoto wengi hawajui madhara ya kukosa elimu bali wazazi wao wanajua hivyo basi wanao uwezo wa kuwaelimisha kwa mifano wanayoijua na inayoonekana katika kusisitiza suala la elimu.
Mama Kikwete alisema, “Tunafahamu fika kuwa katika maandiko yetu na hadith kuwa watoto na mali ni mitihani tuliyopewa na Mwenyezi Mungu na siku ikifika tutaulizwa namna tulivyo wachunga watoto wetu na tulivyotumia mali zetu kwani kuna baadhi ya watu wakipata mali wanamsahau Muumba wao pia hawakumbuki kuwa Mola umpa amtakaye kwa wakati wake yatupasa kuhakikisha kuwa mali haiwi sababu ya kutukosesha pepo”.
Akisoma taarifa ya msikiti huo kwa niaba ya Katibu wa Masjid H. Lufume Mtendaji wa Kijiji hicho Kavindi Salum alisema kuwa miaka ya nyuma waumini wa dini hiyo walikuwa wanaswali ndani ya kibanda cha miti kilichokuwa kimeezekwa kwa makuti lakini mara baada ya ziara ya kikundi cha cha wanawake cha SIRAJAL – MUNIRA kutoka Dar es Salaam kuwatembelea na kuona tatizo hilo waliweza kupatikana wafadhili na kuanza ujenzi.
“Wanandugu wawili kutoka hapa kijijini walitoa eneo lenye ukubwa wa hekari tano na kikundi hiki cha wanawake walitutafutia mfadhili ambaye alitujengea msikiti wa kisasa mwaka 2009 na kutuchimbia kisima kirefu cha maji pia mwaka 2010 ilijengwa madrasa yenye vyumba viwili na mwaka 2011 ilijengwa nyumba ya mwalimu.
Msikiti huo una uongozi wa kamati ya wanaume na wanawake yenye jumla ya wajumbe 22 wanafunzi wa madrasa wavulana 64 na wanawake 79, watoto wanaopata elimu ya awali ni 52 kati ya hao wavulana 36 na wasichana 16 huku idadi ya walimu ikiwa ni wanne kati ya hao watatu wanafundisha dini na mmoja anafundisha elimu ya awali.
Wakati huo huo Mwenyekiti huyo wa kijiji alisema kuwa kijiji hicho kina wakazi wapatao 3,311 ambao wanaabudu katika dini za imani tofauti wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa huduma za afya kwani kina mama, watoto na wazee hutembea umbali wa zaidi ya Km. 28 kufuata huduma hiyo katika eneo la Masaki na kuomba msaada wa kujengewa Zahanati.
“Tunaomba msaada wa kujengewa shule ya Msingi, watoto wetu katika eneo hili hutembea umbali wa zaidi ya Km. tano hadi kufika shule ya msingi Msimbu pia kinamama wanaomba wawezeshwe kifedha na kupewa elimu ya ujasiriamali ili waweze kujikwamua kimaisha”, aliomba Salum.