JK Mjini Windhoek Kuhudhuria Mkutano wa SADC Troika Organ

Mkutano wa Asasi ya Ulinzi, Usalama na Siasa (SADC Troika Organ) wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ukiendelea mjini Windhoek, Namibia.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Windhoek, Namibia, jioni ya Septemba 11, 2013, kuhudhuria Mkutano wa Asasi ya Ulinzi, Usalama na Siasa (SADC Troika Organ) wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Mkutano huo wa siku moja unaofanyika baadaye jioni katika Ikulu ya Namibia mjini Windhoek unahudhuriwa na wakuu wa nchi wanachama wa Troika pamoja na waalikwa kutoka Tanzania, Lesotho, Malawi, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na wenyeji Namibia.

Mkutano huo unafanyika chini ya Uenyekiti wa Rais Hefepunye Phohamba wa Namibia ambaye mwezi uliopita alikabidhiwa Uenyekiti wa Asasi hiyo na Rais Kikwete ambaye aliiongoza kwa mwaka mmoja.

Mbali na Rais Phohamba na Rais Kikwete, viongozi wengine wanaohudhuria mkutano huo ni Rais Joyce Banda wa Malawi ambaye ni Mwenyekiti wa SADC, Rais Joseph Kabila Kabange wa DRC na Waziri Mkuu wa Lesotho Mheshimiwa Tom Thabane.

Hata hivyo, kama mwenyekiti aliyepita, Tanzania inabakia kuwa Mjumbe wa Troika pamoja na Nambia na Lesotho ambayo ni Makamu Mwenyekiti wa sasa wa Asasi hiyo.

Afrika Kusini na DRC zinahudhuria Mkutano huo kama waalikwa hasa kwa sababu moja ya ajenda kuu za kikao hicho ni kujadili hali ilivyo katika Mashariki mwa nchi hiyo ambako majeshi ya Serikali ya Rais Kabila majuzi yalipambana na waasi wa kikundi cha M23 ambacho kinataka kuiangusha Serikali hiyo.

Rais Kikwete na ujumbe wake amewasili mjini Windhoek jioni ya leo akitokea mjini Mwanza ambako asubuhi ya leo amemaliza ziara yake yenye mafanikio makubwa ya siku tano katika Mkoa huo kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.

Kabla ya kuondoka mjini Mwanza, Rais Kikwete amezungumza na viongozi wa Mkoa huo kwenye majumuisho ya ziara yake hiyo.

Kikao hicho pia kitakuwa cha kwanza kwa Katibu Mtendaji mpya wa SADC, Dkt. Stergomena Lawrence Tax wa Tanzania ambaye alichaguliwa mwezi uliopita kushika nafasi hiyo iliyoachwa na Dkt. Tomaz Salamao.