*Ni Tundu Lissu na John Mnyika
*Wawapeleka puta mawaziri
“Waondoa shilingi, CCM wawazidi ujanja
Na Waandishi Wetu, Dodoma
WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu wa Singida Mashariki na John Mnyika wa Ubungo, mwishoni mwa wiki ‘waliliteka’ Bunge wakati wa
mjadala wa Hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Rais Mazingira na Muungano. Hotuba hiyo iliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Lissu na Mnyika walionekana vinara wa mjadala huo wakati Bunge lilipokuwa limekaa kama kamati kupitia makadirio hayo kifungu kwa kifungu.
Dalili za wabunge hao kuteka Bunge, zilianza baada ya Lissu kusimama na kuomba utaratibu kwa aliyekuwa Mwenyekiti ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Katika hoja yake hiyo, mbunge huyo alihoji muda ambao mbunge anatakiwa kutumia anaposimama kutaka ufafanuzi wa jambo fulani.
“Kanuni ya 150 ibara ya 4 inaeleza kuwa kanuni zitatenguliwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
‘Wakati wa kupitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kanuni zilitenguliwa ili wabunge watumie dakika tatu wakati wa kuomba ufafanuzi, lakini kwa leo mbunge akisimama kutaka ufafanuzi anatakiwa aendelee kutumia dakika tano kama kawaida na siyo dakika tatu tena,’ alisema.
Baada ya kauli hiyo ya Lissu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alisimama na kusema uamuzi wa mbunge kusimama na kutumia dakika tatu siyo wa kudumu bali ni wa majaribio ya muda mfupi.
“Labda tu nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kuwa mabadiliko hayo katika kikao chetu cha Kamati ya Uongozi ambacho kwa upande wa Kambi ya Upinzani waliliwakilishwa na Mheshimiwa John Mnyika, tulikubalina mabadiliko hayo yatumike katika siku za mwanzoni baadaye tutakuja ‘ku-revew’ lakini hoja haikutaja mwisho itakuwa lini,”alisema Lukuvi
Baada ya maelezo hayo ya Lukuvi, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika aliomba kutoa taarifa kuhusiana na makubaliano yaliyofanyika katika kikao alichokitaja Lukuvi.
“Katika makubaliano yetu hatukukubaliana kutokutoa hoja ya kutengua kanuni, kwa hiyo kama tunataka kuendelea na makubaliano yetu ilibidi tutoe hoja ya kutengua kanuni,’ alisema Mnyika.
Baada ya mvutano huo, Naibu Spika, Job Ndugai alitoa ufafanuzi kuwa uamuzi uliokubaliwa katika Kikao cha Kamati ya Uongozi ulikuwa wa muda mfupi na wiki ijayo kikao kitakaa tena kufanya tathmini ya utekelezaji wa mabadiliko hayo.
Pamoja na maelezo ya Ndugai, Lissu aliomba mwongozo tena lakini Naibu Spika aliukataa na kuamuru kikao kiendelee.
Wakati huo huo, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), alisimama kutaka ufafanuzi kuhusu viwanda vinavyotoa kemikali kali inayowaathiri wakazi wa Mikocheni Dar es Salaam.
Mdee pia alihoji kama kweli Serikali ya Mapundizi Zanzibar iliiandikia barua Serikali ya muungano kuwa mafuta siyo ya muungano.
Katika kifungu kingine, alisimama Lissu akidai serikali haipo tayari kuwaelimisha watanzania kuhusu muungano.
“Serikali haipo tayari kukiri yale yaliyotokea wakati wa kuanzishwa kwa muungano. Waliokuwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakati huo wako wapi?
‘Mbona hamtaki kusema? Walipotea hivi hivi na haijulikani wako wapi!’ alihoji Lissu.
Akitoa ufafanuzi kuhusu hoja hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Hassan Suluhu, alisema watu waliotajwa na Lissu hata yeye hakuwahi kuwaona badala yake amekuwa akiwasoma katika vitabu.
‘Kama kuna watu walikufa wakati wa kuanzishwa kwa muungano walikuwa ni Wazanzibar. Tuliokaa kitako tukakubaliana kuhusu muungano ni Wazanzibar na kama walikufa kwa muungano tusilifanye jambo hili kuwa la siasa,’ alisema.
Baada ya mjadala huo mjadala mwingine ulioibuka ni baada ya wabunge hao kuhoji ni kwa nini Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Dar es Salaam badala ya Dodoma ambako ndiko yaliko makao makuu ya nchi.
Hoja hiyo ilijibiwa na Kaimu Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, ambaye alisema fedha za ujenzi wa ofisi hiyo zimetengwa kukamilisha ujenzi kwa kuwa jengo limekwisha kuanza kujengwa na hakukuwa na sababu ya kuhamia Dodoma na kuacha jengo likiwa gofu.
Pamoja na ufafanuzi huo, Mnyika alisimama na kuamua kuondoa shilingi katika bajeti ya wizara hiyo kwa kuwa alikuwa hakuridhsihwa na maelezo yaliyotolewa. Hata hivyo hoja yake ilipigwa mweleka baada ya Mwenyekiti kuwahoji wabunge na wengi ambao ni kutoka CCM kusema hawakubaliani na hoja ya mbunge huyo wa chama cha upinzani.
Mjadala mwingine ulioonekana kutikisa Bunge na kutekwa na wabunge hao wawili huku Waziri Samia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk Terezya Huvisa wakiwa katika wakati mgumu wa kutetea bajeti yao ni kuhusu Sh milioni 420 zilizotengwa kwa ajili ya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambazo wabunge hao walisema ni ndogo na haziendani na majukumu ya baraza hilo.
Baada ya mvutano wa hapa na pale, Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (CCM) alijitosa katika mjadala huo na kusema fedha zilizotengwa kwa ajili ya NEMC ni zaidi ya Sh milioni 420.
Lissu alisimama tena na kupinga hoja hiyo na kuhoji mahali fedha hizo zilipoandikwa kwa kuwa katika bajeti zilikuwa hazionyeshwi jambo ambalo alisema anaondoa Shilingi katika bajeti hiyo.
Kama ilivyotokea kwa Mnyika naye alishindwa baada wabunge wengi wa CCM kupingana na hoja yaje wakati walipoulizwa na Mwenyekiti.
Pamoja na mvutano huo uliokuwa ukitawaliwa na wabunge wa CHADEMA huku wabunge wa CCM wakionekana kuwa wasikilizaji kwa asilimia kubwa, wabunge waliidhinisha makadirio ya bajeti ya ofisi hiyo.
Source: Mtanzania