Na Deogratius Temba
MWENYEKITI wa Jukwaa la Katiba nchini, Deus Kibamba, amewataka wanawake nchini kutokubali kuipigia kura rasimu ya katiba mpya iwapo maoni mbalimbali yaliyotolewa na wanawake hasa masuala ya usawa wa kijinsia yasipoingizwa katika rasimu hiyo.
Akitoa mada juu ya mchakato wa katiba ya Tanzania kwenye tamasha la 11 la Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) leo, Kibamba amesema kuwa asilimia zaidi ya 70 wapiga kura nchini ni wanawake hivyo maoni ya wanawake kama hayatasikilizwa na kuwekwa mambo ambayo hayamtetei mwanamke na mtoto katika rasimu hiyo ya katiba basi wanawake nchini wasikubali kuipigia kura ya ndio au hapana kwa rasimu itakayotolewa na tume.
Amasema kuwa mbali ya tume hiyo ya katiba kuwa na wanawake ndani yake ila bado kwa sehemu kubwa wameonyesha kushindwa kupigania maoni ya wanawake kuingia katika rasimu hiyo ya katiba.
Alisema kuwa iwapo tume ya katiba itaendelea na msimamo wake wa kutoingiza maoni sahihi ya wananchi katika rasimu hiyo watambue kuwa hatua ya mwisho baada ya bunge la katiba ni wananchi kuipigia kura katiba hiyo jambo ambalo wananchi wanapaswa kuwa makini na kama itakuwa kimya bila kuingiza masuala ya usawa wa kijinsia .
“ Mchakato huu wa rasimu ya katiba unaendelea ila bado ukitazama vema unaona bado katiba imempa mamlaka makubwa zaidi Rais ya kuteua badala ya kupeleka mamlaka hayo kwa bunge ambalo ni sauti ya wananchi” alisema
Mkurungezi wa TGNP Usu Mallya alisema kuwa baada ya hitimisho la tamasha hilo la 11 washiriki wote zaidi ya 2000 wanaoshiriki tamasha hilo kwa mwaka huu kutoka mikoa mbali mbali Tanzania bara na visiwani watasaini tamko maalum ambalo litaandaliwa na washiriki wa tamasha hilo kuhusu mchakato wa katiba na tamko hilo litafikishwa katika bunge la katiba kama mapendekezo ya wanawake nchini juu ya rasimu hiyo ya katiba.
Kwa upande wake waliyewahi kuwa Waziri wa Maadili na kupambana na Rushwa nchini Uganda, ambaye ni Mwanaharakati wa masuala ya Kijinsia Miria matembe alisema kuwa hakuna katiba bila sauti za wananchi wote na kuzingaitia uasawa wa Kijinsia.
“Ni lazima mchakato uzingatie uasawa wa Kijinsia, wasililize sauti za wanananchi wanapendekeza nini na wanataka kitu gani kingie kwenye katiba yao”alisema
Akizungumzia kuhusu kutokuwepo kwa jina la nchi ya Tanganyika katika rasimu ya Katiba Mpya, matembe alisema kuwa huwezi kuwa na Tanzania bila kuitaja Tanganyika na lazima watanzania wajiulize ndo akti ya Zanzibar iliyo zaa Tanzania ilifungwa na nani?
“Sitaki kuingilia masuala haya ya ndani ya nchi yenu, lakini wahuisika ni lazima wajue kuwa hakuna sababu ya kufunga watu midomo wasijadili jina la nchi yao, wau kujua mustakabali wa Muungano wa nchi zao. Sambamba na hayo ni lazima kuangalia suala la uwepo wa sauti za wananchi..”alisema.
Kwa upande wake Mwezeshaji kutoka katika Shirika la Plan Internation
Anna Mushi alisema kuwa mfumo wa kutopata Elimu ya afya ya uzazi kwa watoto ndio chanzo kikubwa cha mimba za utotoni.
Alisema kuwa hatua ya kutunga katiba imefikia kwa kuuundwa kwa bunge maalum la katiba ambapo kwa mujibu mswada uliowasilishwa bungeni jana (juzi) unampa madaraka rais kuteua wajumbe 166 kutoka katika makundi mbalimbali na wabunge wote 357 kutoka Tanzania bara na 81 kutoka Visiwani hali ambayo inaonyesha katiba itakayopatikana itakuwa ya upande mmoja.
“Kilichotakiwa kufanyika ni rais kutoa ridhaa kwa Watanzania kuwachagua wawakilishi wao kutoka katika kundi husika na wananchi ndiyo wanastahili kuwa na idadi kubwa katika bunge hilo badala ya wabunge kuwa wengi zaidi kama ilivyopendekezwa katika Muswada huo” alisema.