NDEGE ya abiria iliyokuwa na watu 112 imeanguka kwenye uwanja wa ndege wa Kisangani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Takriban watu 40 wamekutwa wakiwa hai, lakini wengine zaidi ya 50 wanasemekana kufariki dunia. Ndege hiyo, iliyo chini ya shirika la ndege la Hewa Bora, ilijaribu kutua baada ya hali ya hewa kuwa mbaya ikitokea Kinshasa.
Hakuna uthibitisho bado wa aina ya ndege iliyohusishwa. Mkurugenzi mkuu wa Hewa Bora Stavros Papaioannou aliliambia shirika la habari la Reuters, ” Rubani alijaribu kutua lakini hakufanikiwa kugusa barabara ya ndege.”
Msemaji wa serikali Lambert Mende alisema ndege hiyo iligonga karibu sana na uwanja wa ndege huku kukiwa na radi. Alisema; “Tumejitahidi kuwaokoa watu 40 na harakati za uokoaji zinaendelea”.