Halima Mdee amlipua kigogo wa Wizara ya Ardhi

Dodoma
MBUNGE wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee amemlipua kigogo mmoja wa, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kwa madai kuwa anamkingia kifua, Robert Mugisha anayejenga katikati ya mto na hivyo kusababisha kero kwa wakazi wa Kawe Darajani.

Amedai kuwa, Mshumbusi anaendelea na ujenzi huo kwa kutumia hati isiyohalali aliyopewa na kigogo huyo. Mdee alitoa kauli hiyo Bungeni jana, wakati akichangia hotuba ya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2011/2012, na kueleza kuwa licha ya Mugisha kupewa ‘stop order’ lakini yeye anaendelea tu na ujenzi.
“Katika jimbo langu maeneo ya wazi yameuzwa na kuna mjanja amejenga maghorofa na hivyo kusababisha mifereji kuziba na kuwapa kizaazaa wananchi pindi mvua zinaponyesha.
…Katika eneo la Bonde la mpunga mvua inaponyesha panatisha, kuna kigogo mmoja wa ardhi na Baraza la Mazingira Tanzania (NEMC), wanashikishwa fedha na kuacha ujenzi uendelee.
…NEMC kila wanapokwenda wanashikishwa fedha na kurudi bila kuchukua hatua yoyote, sasa nataka kujua nini mustakari ya watu wa Bonde la mpunga,” alihoji Mdee.
Mdee akiendelea kuchangia aliwataka mawaziri kutimiza majukumu yao na si kufanya kwa ujiko (sifa).
“Tusiwe mawaziri kwa ujiko tekelezeni kazi zenu. Viwanda vinajengwa na kutiririsha maji kwenye makazi ya watu bila kuchukua hatua za kusimamisha ujenzi huo.
…Hivyo mawaziri timizeni majukumu yenu kwa kusimamisha ujenzi huu na uchafu udhibitiwe bila kuathiri mazingira,” alisema.
Akizungumzia kuhusu muungano alisema kuna kero 13 lakini kati ya hizo ni mbili tu ndizo zimeshughulikiwa na kuongeza kuwa kuna haja ya kushughulikia kero za muungano likiwemo suala la mafuta.
Mdee aliongeza kuwa “muungano una kero nyingi lakini jambo la kushangaza ni kwamba tangu Rais Kikwete ameingia madarakani vimefanyika vikao sita tu”
“Tutafute suluhu kwenye suala la mafuta, sisi tuna madini lakini wenzetu hawajawahi kuhoji sisi likija suala la mafuta tuko mbio mbio. Pia vikwazo kwenye Katiba mpya lisiwekwe, watu waachwe wajadili.
…Mambo ya funika kombe mwanaharamu apite hayafai, na hili ndilo limesababisha muswada wa katiba urudishwe kutokana na wenzetu kutoshirikishwa,” aliongeza.