By Isaac Mwangi,EANA
JUMUIA ya Afrika Mashariki (EAC) hivi sasa inajikita katika utafiti wa uelewa wa wananchi wa kanda hiyo juu ya jumuiya hiyo, utafiti ambao unatarajiwa kuimarisha uaminifu wa mtangamano na kugusa mionyo na mawazo ya raia mwa kanda hiyo.
Katibu Mkuu wa EAC, Dk Richard Sezibera alisema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa anazindua rasmi utafiti huo wa ndani na nje ya mtandao kwa mwaka 2013.
Akihutubia wageni makao makuu ya jumuiya hiyo jijini Arusha, Dk Sezibera alisema utafiti huo kwa njia ya mtandao unawalenga wafanyakazi wote wa EAC ikiwa ni pamoja na taasisi na asasi zake na wizara za masuala ya Afrika mashariki katika nchi wanachama bila kujali nyadhifa zao.
Utafiti huo pia unalenga wadau wa ndani na nje ya kanda hiyo. ” EAC inafanya utafiti ili kuweza kubaini jinsi EAC inavyoeleweka na wadau na jumuiya yenyewe kwa ujumla wake,”
Utafiti huo unafanyika kwa msaada wa Shirika la Misaada la Kimataifa la Ujerumani (GIZ).
Dk Sezibera lisema utafiti huo umegawanywa katika awamu nne ikiwa ni pamoja na kutathmini mahali ilipo EAC sasa, wapi EAC inataka kuelekea, namna ya kufika huko na mwisho utekelezaji, usimamizi na kufanya tathmini.
Naye Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Masuala ya Umma wa EAC, Richard Owora aliwambia wageni hao kwamba utafiti huo unajumuisha mambo mablimbali ikiwa ni pamoja na ziara ya mafunzo,madodoso kwenye mitandao, mahojiano ya ana kwa ana na kura za kwenye mtandao kupitia tovuti na mtandao wa facedebook wa EAC.