Na Mwandishi wa EANA, Arusha
KIKAO cha Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kilimalizika mwishoni mwa wiki kwa bunge hilo kupitisha sheria mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya kuifanya Novemba 30 ya kila mwaka kuwa siku ya mapumziko kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Sheria hiyo ya Siku ya Mapumziko kwa EAC ya mwaka 2013 ina maanisha kwamba tarehe hiyo itakuwa ni siku ya mapumziko kwa nchi zote tano za jumuiya hiyo ambazo ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.
Kama wakuu wa nchi wanachama wakiridhia sheria hiyo, siku hiyo itakuwa ni nafasi muhimu ya kutathmini mwelekeo wa mtangamano na kufurahia mafanikio yalikwishafikiwa pamoja na shughuli na mipango inayoendelea juu ya kufikiwa kwa malengo ya Mkataba wa EAC.
Wakati huohuo sherehe rasmi itakuwa inaazimishwa kwa mzunguko kwa zamu miongoni mwa nchi wanachama, kusherehekea kuzaliwa upya kwa jumuiya na kuwatambua waliopigania kuanzishwa kwa mtangamano huo.
Mswada wa sheria hiyo ulisomwa na Mheshimiwa Mike Sebaku kwa niaba ya Mheshimiwa Abubakar Zein Abubakar,unatarajiwa kuweka msingi wa siku ya mapumziko katika Jumuiya na pia kuweka kipengele cha posho kwa watumishi wa EAC ambao huenda wakahitajika kufanyakazi siku hiyo ya mapumziko pamoja na kuweka utaratibu iwapo siku hiyo itaangukia siku ya Jumapili.
Sheria hiyo pia inatambua siku zote za maazimisho ya siku za uhuru kwa kila nchi mwananchama kuwa ni siku za mapumziko kwa wafanyakazi wa Jumuiya na taasisi zake zote.Pia sheria hiyo inatambua siku za mampumziko za sherehe za dini ikiwa ni pamoja na Ijumaa Kuu, Pasaka na Idi zote. Nayo Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani ambayo huazimishwa Machi 8, ya kila mwaka nayo inatambuliwa kuwa ni miongoni mwa siku za mapumziko kwa EAC.
Wakati wa mjadala, mswada huo uliuungwa mkono na waheshimiwa Patricia Hajabakiga, Dora Byamukama, Peter Muthuki na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri, Mheshimiwa Shem Bageine. Kupitishwa kwa mswada huo sasa kunasubiri baraka za wakuu wa nchi wanachama kuupitisha ili uwe sheria kamili ya EAC.